15 February 2013

USITISHAJI MATANGAZO BUNGENI Ofisi ya Bunge yapingwa vikali *Wananchi wahoji siri inayotaka kufichwa *Wabunge washauriwa kususia vikao bungeni


Na Waandishi Wetu

SIKU moja baada ya Ofisi ya Bunge, kuvunja ukimya na kudai inaangalia uwezekano wa kusitisha matangazo ya moja kwa moja katika vikao vya Bunge kwa njia ya televisheni mjini Dodoma ili kudhibiti vurugu za wabunge wanaodaiwa kutafuta umaarufu,
hatua hiyo imepingwa vikali na watu mbalimbali.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, walisema Bunge linaendeshwa na kodi za wananchi hivyo ni haki yao
kuona kinachoendelea wakati vikao vikifanyika.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini, Dkt. Valentino Mokiwa, alisema kitendo cha Ofisi ya Bunge kutaka kuzuia matangazo hayo anakifananisha na baba, mama kujifungia
chumbani na kuanza kupigana ili watoto wasiwaone.

“Tunapenda kuwaona wabunge wakiwa wanalala bungeni bila kuchangia mada yoyote, wengine wakichezea simu zao bila kufuatilia kinachoendelea,” alisema Dkt. Mokiwa na kuongeza kuwa, hakuna sababu ya Watanzania kunyimwa uhondo.

Alisema suluhisho la mambo yanayotokea bungeni si kuzuia matangazo hayo yasirushwe moja kwa moja bali wenyewe
wanapaswa kujirekebisha, kuelewana na kuzungumza
mambo yenye kuleta ufanisi kwa jamii.

Alisema lazima ifahamike kuwa, Bunge ni vikao vitakativu vya Taifa hivyo kila mwananchi anapaswa kuona kile kinachoendelea bungeni.

Padri Mapunda

Kwa upande wake, Padri wa Kanisa Katoliki Baptiste Mapunda, alisema uamuzi huo ni kielelezo kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinawaogopa wapinzania ambao wanaonekana kuwa na hoja nzito zinazohitaji majibu ya Serikali.

“Bunge ni la Watanzania wote si la chama kimoja cha siasa hivyo wananchi wana haki ya kuona kama kuna upuuzi unafanyika katika vikao hivyo, hatuwezi kurudi katika ukoloni,” alisema na kuongeza.

“Hata Biblia inasema mtu anayependa mambo ya giza ni muovu... kwa uamuzi wanaotaka kuufanya ni sawa na kutuambia kuna
maovu ndani yake wanayaficha,” alisema Padri Mapunda.

Aliongeza kuwa, Tanzania kuna wasomi hivyo uamuzi wanaotaka kuufanya ni aibu kwa nchi na ukiukwaji wa uhuru wa habari.

Mchungaji Mtikila

Naye Mwenyekiti wa Chama Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, alipinga mpango huo na kudai Bunge si la wabunge bali ni mali ya wananchi hivyo ni haki yao kuona kila kinachoendelea bungeni.

“Wananchi ndiyo waliowapa wabunge fulsa ya kuingia bungeni, kitendo cha matangazo ya moja kwa moja kutorushwa katika televisheni, wabunge wanapaswa kugoma wasiingia katika
vikao hadi uamuzi huo utakapotenguliwa,” alisema na
kuongeza kuwa, kauli ya Dkt. Kashilila, amempotezea
sifa ya kushika wadhifa huo.

CHADEMA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema wananchi waamue kile wanachokitaka na chama hicho kitakuwa mstari wa mbele kushirikiana nao.

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano, wa cham hicho Bw. John Mnyika, alisema wananchi ndiyo walipa kodi hivyo Serikali haiwezi kuwazimia matangazo wakati wa Bunge na kufanya hivyo ni kuwanyima haki ya kupata habari.

Kituo cha LHRC

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dkt. Helen Kijo-Bisimba, alisema Dkt. Kashilila hajui anachokisema kwani kuna demekrasia za aina mbili.

Alizitaja demokrasia hizo kuwa ni ile ya moja kwa moja na uwakilishi hivyo matangazo ya televisheni ni ya uwakilishi
kwani si watu wote wanaweza kwenda bungeni.

Alisema hata televisheni moja inayoonesha haitoshi badala yake ingetakiwa luninga zote zioneshe na kusisitiza kuwa, wabunge hawakutumwa bungeni kulala bali wafanye kazi.

NCCR Mageuzi

Chama cha NCCR-Mageuzi, nacho kimedai kusikitishwa na taarifa
ya Dkt. Kashilila kudaio Ofisi ya Bunge inaangalia uwezekano wa kutorusha matangazo ya televisheni moja kwa moja katika vikao
vya Bunge badala yake vitafanyiwa uhariri na kuchujwa kabla
ya kuwafikia wananchi.

Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw. Faustin Sungura, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na
waandishi wa habari.

Alisema chama chake kinapinga kwa nguvu zote hatua zozote zinazotaka kuchukuliwa na mamlaka yoyote kuzuia matangazo
ya vikao vya Bunge yasirushwe moja kwa moja.

Aliongeza kuwa, vurugu zinazodaiwa kutokea bungeni haziwezi kukomeshwa kwa kuzuia matangazo hayo yasirushwe moka kwa moja bali zinaweza kukomeshwa kwa utaratibu wa kawaida unaotokana na kanuni.

“Kuzuia matangazo ya moja kwa moja kupitia luninga, hakumzuii mbunge anayejisikia kuzungumza analotaka pia hakuzuii baadhi ya wabunge kutafakari kwa makini, kutumia muda mwingi kwenye simu zao za mikononi badala ya kuwawakilisha wananchi.

“Mawazo ya Katibu wa Bunge hayalengi kuzuia vurugu bali kuzuia watu walio nje ya bunge wasione vurugu hiyo haina tofauti na mtu kuvaa nguo mpya juu ya mwili mchafu,” alisema.

Bw. Sungura alisema, mawazo hayo yanakinzana na ibara ya 18 (d) ya Katiba ya nchi inayosema kila mtu anayohaki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha, shughuli za wananchi na jamii,” alisema.

Aliongeza kuwa, chama hicho kinaamini kuwa matukio yote yanayotokea bungeni kama kufanya fujo, kulala usingizi, kuchezea simu badala ya kusikiliz ahoja, kuzungumza hovyo bila utaratibu, Spika na Naibu wake kushindwa kuendesha Bunge ni mambo muhimu ambayo wananchi wanapaswa kuyajua.

Profesa Baregu

Madhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustine (SAUT),
Profesa Mwesiga Baregu, alisema hakufikilia kama Dkt. Kashilila kuzungumza maneno yanayoweza kusababisha maandamano.

Alisema matangazo ya vikao vya bunge kurushwa moja kwa
moja, yamewasaidia baadhi ya wabunge kujirekebisha.

“Wale waliokuwa wanalala wamepunguza, watoro sasa wanahudhuria vikao hivyo ni wazi wamebadilika...ni vyema
jambo zito kama hili lisiamuliwe na mtu mmoja,” alisema.

Habari hii imeandikwa na Rose Itono, Rehema Maigala na Peter Mwenda.



5 comments:

  1. haki ya mungu huyo dkt ni mwehu ananza kuchanganyikiwa hao ndo wasio tufa walioingia kwa rushwa katika madaraka sasa anaanza kuaibika yaani kama ni mzoga umeanza kutoa harufu na wadudu

    ReplyDelete
  2. HATUA YA WABUNGE VIJANA KWENDA JKT IUNGWE MKONO NA MAKUNDI YOTE YA WALE AMBAO HAWAKUPITIA JUKWAA LA WANAHABARI,WANAHARAKATI WA HAKI ZA BINADAMU NAUTAWALA BORA ,TAMWA NA WAHADHIRI WA VYUO VIKUU VYOTE NCHINI TUNA MATUMAINI MAFUNZO YALIYOKAMILIKA NI YALE YANAYOSABABISHA BADILIKO LA TABIA LA KUDUMU AMBALO NI ENDELEVU TUWE WAZALENDO KAMA CHINA,CUBA KOREA YA KASKAZINI NA ISRAEL

    ReplyDelete
  3. Kutokuonyesha vikao vya bungeni ni sawa na walewale waliokuwa wanasema mikataba tena ambayo wananchi wamegundua ni bomu, ya ufisadi ni S I R I. Katibu wa bunge anataka kuficha maovu bungeni kama kulala, kushangilia hoja badala ya kuchangia meaningfully, mikatana kama ya gesi ndiyo ya kuangalia kwa makini bila hivyo nchi yetu itauzwa nasi pamoja na vizazi vyetu kubaki watumwa mpaka kiama. Hawa ndiyo viongozi, watalaamu wetu waliosoma UDSM kitivo cha sheria -- copy and paste projects as a result mikataba ya kifisadi mradi kupata gari la kutembelea na watoto kusomeshwa nje.

    ReplyDelete
  4. Dkt. Kashilila anaelekea pabaya kutaka kuturudisha enzi za "manual' wakati sasa dunia inaelekea kwenye mfumo wa 'Digital'. Huko ni kuishiwa maneno ya kuzungumza mbele ya jamii.

    ReplyDelete
  5. UTANDAWAZI HAUKWEPEKI SI RAHISI KUMZUIA NDEGE ASIRUKE JUU YA KICHWA CHAKO ILA UTAKUWA PUNGUANI NAMBARI WANI KUMRUHUSU NDEGE ATUE NA KUJENGA KIOTA JUU YA KICHWA CHAKO AKAJENGA KIOTA ,AKATAGA NA KUANGUA VIRANGA WEWE UKICHEKELEA SISI SIO SPONJI WA KUNYONYA KILA UCHAFU WA UTANDAWAZI IKIZINGATIWA TUNA WANAFALISAFA WACHACHE WANAOWEZA KUTABIRI KESHO YA WATANZANIA ITAKUAJE ,WENGI HATA JUZI TU SEMBUSE JANA WALISHANGAA IKITOKEA HIVYO SIDHANI KUNA KITU KINACHOFICHWA LA MSINGI TUNAJENGA KIZAZI GANI CHA KESHO MFANO HATA LEO AKIZALIWA KICHANGA PALE PALESTINA AMEJAZWA SUMU KUWA WAISRAEL NI ADUI ZAO JE KIZAZI CHA TANZANIA KINAAMINISHWA NA KURIRITHISHWA UPUUZI ULE UNAOFANYIKA BUNGENI ANGALAU WANGEKUWA WASTAARABU SINA UHAKIKA IWAPO ATHARI ZA MMOMONYOKO WA MAADILI BUNGENI UTAONEKANA LEO NI MIAKA MIONGO MIWILI HADI MITATU KIZAZI CHA LEO KITAKUWA HAKIPO NI WALE WANAOAMINI DUNIA NI UWANJA WA FUJO KWA HIYO UNYESHA RAFU ZAKO KISHA ISHIA KUZIMU KIZAZI KIJACHO WATAJIJU HUO NI UJAMBAZI WA HALI YA JUU SINA UHAKIKA IWAPO NITAELEWEKA MWENYE MASIKIO AHURUMIE KIZAZI KIJACHO

    ReplyDelete