07 February 2013

Uchaguzi Mkuu TAFCA kufanyika Machi 16


Na Mwandishi Wetu

BAADA ya Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Makocha Tanzania (TAFCA), kukwama mara mbili, wanachama wa chama hicho wamepewa fursa ya kufanya uchaguzi wa chama hicho Machi 16, mwaka huu mjini Dodoma.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Ofisa Habari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Boniface Wambura, tangazo la uchaguzi huo limeeleza kwamba fomu kwa ajili ya waombaji uongozi katika TAFCA zitaaza kutolewa leo na mwisho wa kurudisha ni Februari 11 mwaka huu.

Wambura alisema majina ya waombaji uongozi, watakaokuwa wamepitishwa yatatangazwa Februari 12 mwaka huu.

Alisema kipindi cha kuweka pingamizi ni kuanzia Februari 13 hadi 17 mwaka huu. Usaili kwa waombaji utafanyika Februari 19 mwaka huu wakati matokeo ya usaili yatatangazwa Februari 20 mwaka huu.

Alisema Kamati ya Uchaguzi ya TFF itasikiliza rufaa kama zitakuwepo kati ya Februari 20 na 22, mwaka huu na uamuzi wa rufaa hizo utatangazwa kati ya Februari 23 na 27 mwaka huu.

Wambura alisema ada za fomu kwa waombaji uongozi zitakuwa sh. 200,000 kwa nafasi zote isipokuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na wajumbe wa Kamati ya Utendaji.

Alisema nafasi zitakazowaniwa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mhazini, Mhazini Msaidizi, Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF na wajumbe wa Kamati ya Utendaji.

Ofisa huyo alisema fomu kwa waombaji uongozi zinapatikana kwenye ofisi za TAFCA, zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment