07 February 2013

TBF yaivunja timu ya Taifa



Na Amina Athumani

SHIRIKISHO la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), limeivunja timu ya Taifa na sasa itachagua wachezaji wengine katika Ligi Mpira wa Kikapu (NBL).


Timu hiyo imevunjwa, baada ya kufanya vibaya katika michuano ya mchezo huo Kanda ya Tano 'Zone V', iliyomalizika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Ligi ya NBL, inatarajia kufanyika Aprili mwaka huu ambayo itashirikisha timu bingwa za kila mkoa, ambao kila mmoja utawakilishwa na timu aa wanawake na wanaume.

Akizungumza na gaazeti hili Dar es Salaam jana Makamu wa Rais wa TBF, Phares Magesa alisema kikosi kitakachochaguliwa upya, kitakachoingia katika mafunzo ya muda mrefu, yatakayoendeshwa na makocha wa kigeni kutoka nchini Marekani.

"Tuna programu ya muda mrefu, ambayo itaendeshwa na makocha hawa wa kigeni kutoka nchini Marekani, Albert Sokaitis wa Post University ambaye ni Kocha Mkuu na Kocha Msaidizi wa timu yetu Jocquis Sconiers," alisema Magesa.

Alisema Program hiyo itakuwa ni ya miaka minne, ambapo pia itaendeshwa kwa ushirikiano na makocha wazalendo wa hapa nchini.

Magesa alisema cha msingi ni mikoa kuhakikisha inawapa maandalizi ya kutosha timu zao, ili kushiriki kikamilifu katika ligi hiyo na kupata wachezaji wenye viwango.

Alisema mpaka sasa ipo mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na mingine ambayo imefanya mashindano yao na kupata mabingwa wake.

"Ile ambayo bado haijafanya, inatakiwa hadi ifikapo Machi mwaka huu, iwe tayari imewasilisha majina ya timu zao zitakazoshiriki michuano hiyo ya Klabu Bingwa Tanzania," alisema.

No comments:

Post a Comment