18 February 2013

Tume ya Katiba yapongezwa


Na Peter Mwenda

JUKWAA la Katiba Tanzania (JUKATA) limeipongeza Tume ya Katiba ya Mwenyekiji Jaji Joseph Warioba kutoa muongozo wa kupata katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini imekosoa utaratibu wa kupata wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa kuwaingiza moja kwa moja kwa nyadhifa zao madiwani wote 4,453 nchini.


Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Bw. Deus Kibamba akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam alisema kuwa madiwani walichaguliwa kwa ajili ya kuwakilisha wananchi katika ngazi mbalimbali lakini hawatakiwe wawepo katika kuwakilisha mabaraza ya katiba.

Alisema uwakilishi wa madiwani kwenye mchakato wa Katiba utaleta mgongano wa itikadi za vyama vilivyowaweka madarakani hivyo kuleta msigano kwenye mabaraza ya katiba na kujenga uhasama kati yao na wabunge kipindi cha kuomba kura kwa wananchi kinapofika.

Bw. Kibamba alisema majukumu hayo madiwani ni kuwalundikia kazi kama walivyowahi kulalamika na kuongeza kuwa kutaingilia wajibu wao kama wenyeviti wa Kamati za Maendeleo ya Kata.

Alisema nafasi za madiwani zichukuliwe na wajumbe wanane kutoka katika kila Kata na majumbe wengine kutoka Asasi za Kiraia kama walemavu.

Bw. Kibamba alisema kasoro nyingine ni kuwa sifa za kuchaguliwa kuwa wajumbe wa baraza la katiba la wilaya ni lazima awe raia wa kuzaliwa wa Tanzania lakini hiyo haitoshi kwa vile raia wameandikishwa hivi karibuni na miaka mingi lakini uzalendo wa baadhi yao una mashaka.

Alisema wajumbe hao ni vyema wawe watanzania kwa kuzaliwa kwao na wazazi wao na jamaa zao wawe wanajulikana kuwa raia wazawa wa Tanzania na awe mkazi wa kudumu wa kijiji, mtaa au shehia kwa wale wa Zanzibar.


Bw. Kibamba alisema utaratibu wa kuwapata wajumbe kwenye mabaraza ya Katiba ya Ngazi ya Wilaya na Serikali za Mitaa Mabaraza hayo wawe wazi kwa kupiga kura ya uwazi kupunguza malalamiko na migogoro inayoweza kujitokeza.

Alisema kuwa Tume hiyo pia iseme kwenye muongozo huo kuwa mabaraza ya Katiba yatakaa madarakani kwa muda gani njia zitakazotumika endapo zitakuwa za kuwafuata wananchi majumbani, kwenye ukumbi mmoja au kuhama hama na madaraka ya watendaji wa vijiji na Masheha lazima yawe na ukomo.

No comments:

Post a Comment