18 February 2013

Wakazi Keko kulipwa fidia



Na Goodluck Hongo

BAADHI ya wakazi wa Keko Machungwa Bondeni wameanza kulipwa fidia ya nyumba zao ili wahame katika sehemu ambayo hujaa maji ya mvua kutokana na kuzibwa kwa mtaro wa kupitishia maji na mmiliki wa Kampuni ya mafuta ya Oil Com baada kujenga ghala katika eneo hilo.

Akizungumza na Majira Dar es Salaam juzi Ofisa Habari wa Manispaa ya Temeke Bi.Joyce Msumba alisema mgogoro katika sehemu hiyo umeanza siku nyingi kati ya wakazi wa eneo hilo na mmiliki wa oil com ambaye anadaiwa kujenga na kuhamisha mtaro wa maji na kuuelekezea kwa makazi ya wananchi.

Alisema wiki chache zilizopita nyumba zaidi ya  kumi kati ya 29 zimeshalipwa tayari na waliobaki watalipwa mwisho wa mwezi huu ili wahame kutoka katika sehemu hiyo.

"Tumekwenda eneo hilo tumejionea na pia tulikwenda kuonana na uongozi wa kampuni ya Oil Com ambao ndio walipaji na wao wametuthibitishia kuwa ifikapo mwisho wa mwezi huu watamalizia nyumba zote zilizobaki, kwani mgogoro katika sehemu hiyo ni wa siku nyingi sana,"alisema.

Alisema tathmini iliyofanyika kwa nyumba zote katika eneo hilo zilitakiwa kulipwa jumla ya nyumba zote zaidi ya sh.milioni 900 ambapo walitakiwa kulipwa kwa awamu tofauti.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Bw.Photidas Kagimbo alisema anafahamu kuhusu eneo hilo na kwamba alikuwepo siku ambayo wakazi hao walilipwa wiki mbili zilizopita

"Ni kweli nalifahamu swala hilo vizuri tu na tena wiki mbili zilizopita nilikuwepo wakati wa kikao wakipewa cheki zao kwa baadhi ya nyumba, lakini hilo mkienda kwa Ofisa habari wa Manipsaa atawapa habari kamili. 

Majira ilifuatilia sakata hilo kwa muda mferu ambapo wakazi wa eneo hilo walidai kuwa walitakiwa kulipwa pesa zao tangu mwezi wa sita mwaka jana lakini hadi kufikia leo hii hawajui lini watalipwa fedha zao

Mkazi mmoja wa eneo hilo aliyejulikana kwa jina moja la Makinda alisema kuwa ingawa hilo limetokea lakini nyumba zilizolipwa ni za kuchagua kwani walitakiwa kulipwa mapema fedha hizo ili wahame.

Alisema swala la kulipwa kwao ni la muda mrefu na linajulikana hadi kwa Ofisi ya Waziri Mkuu,Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa hadi Wilaya na limekuwa na sintofahamu kutokana na wakazi hao wengi kutojua nini kinachoendelea kwani aliyesababisha madhara hayo yupo lakini inachukua muda mrefu sana kuwalipa 

Awali katika sakata hilo inadaiwa kuwa mmliki wa kampuni wa oil com ambaye amejenga katika sehemu hiyo na kuziba mfereji wa maji na kusababisha maji yote yanayotoka katika barabara ya kilwa road kujaa katika makazi ya watu hao hali inayoweza kusababisha maafa na magonjwa ya mlipuko kwa wakazi wa eneo hilo.

Majira lilimtafuta mkurugenzi wa kampuni ya Oil Com inayolalamikiwa ili kuelezea sakata hilo na kutolea ufafanuzi ahadi yake ya kuwalipa wakazi waliobaki ifikapo mwisho wa mwezi huu hazikufanikiwa kutokana na walinzi wake wa mlangoni kusema kuwa yupo nje ya nchi na atarudi baada ya wiki moja

No comments:

Post a Comment