20 February 2013

TGNP wapinga kuvunjwa POAC


Na Mariam Mziwanda

MTANDAO wa Jinsia nchini (TGNP), umetoa tamko la kulaani kitendo cha Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda, kuifuta Kamati
ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC).


Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji TGNP, Bi. Lilian Liundi ilisema Bunge ni baraza ambalo mamlaka yake yapo kwa wananchi
hivyo viongozi wake wanapaswa kutambua kuwa, wao ni
wasimamizi wa vikao vya baraza hilo si vinginevyo.

Aliongeza kuwa, TGNP imeshtushwa pia na kitendo cha Bi. Makinda kuifuta kamati hiyo POAC, ambayo ilikuwa na ufanisi mkubwawa kudhibiti mianya ya ufisadi katika sekta ya umma.

“Sisi kama wanajamii, tutaendelea kudai ulinzi wa rasilimali za Taifa letu kwani kamati hii ni muhimu irudishwe...mashirika ya umma yaliyopo nchini ni 258 yenye dhamani ya sh. trilioni 10.2.

“Tunahitaji kamati makini ya Bunge ili kunusuru rasilimali hizi vinginevyo Taifa litakwama kupiga hatua ya maendeleo,” alisema
na kuongeza kuwa, kama kamati hiyo isiporudisha, wizi wa fedha
za umma utarudi kwa kasi kama ilivyokuwa zamani hivyo
wangependa kuona POAC ikirudishwa Aprili mwaka huu.

Bi. Liundi alisema, Bunge linapaswa kutuwakilisha ipasavyo na kudai uwajibikaji wa watendaji serikalini ambapo TGNP imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya Ofisi ya Bunge kudai ilikuwa inaangalia uwezekano wa kusitisha matangazo ya moja kwa moja katika vikao vya Bunge mjini Dodoma kwa njia ya televisheni.

Alisema hatua hiyo imelenga kuwanyima wananchi fursa ya kufuatilia mijadala inayowahusu na kujiridhisha kama wabunge
wao wanafikisha kero zao kama wanavyotaka.

“Serikali ya Tanzania imeridhia tamko la Haki za Binadamu la Desemba 10,1948, ambapo kifungu cha 19 cha tamko hili, kinatoa
uhuru wa mtu kutoa, kupokea mawazo bila kujali mipaka ya nchi
ambapo haki ya kutoa mawazo haipaswi kuingiliwa,” alisema.

2 comments:

  1. Mhe Makinda kaelekezwa na viongozi mafisadi ndani ya serikali ya Rais Kikwete kufutilia mbali POAC ili waendelea kuchukua vyao kabla ya 2015 lakini sisi raia wa kawaida tunaimani kuwa baada ya uchaguzi wa 2015 viongozi hawa wote watashikwa pamoja ya spika Makinda kama mshiriki wao mkuu,awamu kama ya marehemu E Sokoine itaingia madarakani, Mungu ni Mkubwa na ana huruma na taifa hili la Tz.

    ReplyDelete
  2. HAKUNA MWENYE HATI MILIKI YA KAMATI YO YOTE NANI ALIJUA DR.MWAKYEMBE ATANG'AA WIZARA YA UCHUKUZI

    ReplyDelete