11 February 2013

'Serikali itazame upya adhabu kwa wanaonyanyasa wanawake, watoto'



Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imeshauriwa kuzitazama upya adhabu zinazotolewa
kwa watu wanaotiwa hatiani kutokana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.


Hali hiyo inatokana na ongezeko la vitendo hivyo pamoja na wahusika kupewa adhabu ndogo hivyo jamii kuona ni jambo
la kawaida kufanya unyanyasaji kwa watu wengine.

Waziri wa Kazi na Ajira, Bi. Gaudensia Kabaka, aliyasema hayo mjini Dodoma jana wakati akizungumza na waandishi wa habari
juu ya uzinduzi wa “Kampeni ya Okoa Mtoto na Kike Tanzania”
inayoratibiwa na Kampuni ya Nyumbani Kwanza Media Group
(NMG).

Kampeni hiyo itazinduliwa katika Wilaya ya Tarime, mkoani
Mara na baadaye kusambaa katika maeneo mengine nchini hasa yanayotajwa kushamiri kwa vitendo hivyo.

Bi. Kabaka ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu mkoani
Mara, alisema vitendo vya unyanyasaji kwa wanawake na watoto, havikubaliki na adhabu kali zinapaswa kutolewa kwa wahusika ambapo pamoja na kuwepo sheria na adhabu kutolewa, bado
unyanyasaji umeshika kasi katika maeneo mengi.

“Unyanyasaji umeshika kasi kwa kiwango cha ajabu na unarudisha nyuma maendeleo ya Taifa na ya wanawake nchini, sheria ipo na adhabu zinatolewa lakini nadhani kuna udhaifu mahali.

“Kuna kila sababu ya kuangaliwa upya sheria husika ili kukomesha vitendo hivi, zaidi ya moja ya tatu ya wanawake wamekabiliana na ukatili wa kijinsia na mgawanyo wa unyanyasaji ni mkubwa hasa
kwa wanawake waliotalikiwa na wajane,” alisema.

Aliongeza kuwa, utafiti unaonesha asilimia 23 ya wasichana
wenye umri kati ya miaka 15 hadi 19, tayari wamejifungua hivyo kushindwa kuendelea na masomo kwa ajili ya kuajiandaa na
maisha yao ya baadaye.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Mossy Magere, alisema kampeni hiyo itazinduliwa rasmi Machi 3 mwaka huu na kusisitiza kuwa, ameamua kumshirikisha Bi. Kabaka kwa kuwa yupo mstari
wa mbele kutetea haki za wanawake.

“Tatizo la unyanyasaji kijinsia ni kubwa mkoani Mara na kampeni hii itakuwa endelevu ikienda sambamba na uanzishwaji wa klabu
za kupinga unyanyasaji katika shule mbalimbali ili kuleta usawa.

“Unyanyasaji wa kijinsia unaumiza wanawake na watoto wengi nchini hivyo lazima jamii ikubali kubadilika ili kila mtu awe na furaja katika maisha badala ya wengine kujuta kuzaliwa,” alisema.

No comments:

Post a Comment