11 February 2013

Watendaji CCM wajiuzulu kwa shinikizo la wananchi


Na Yusuph Mussa, Korogwe

MWENYEKITI wa Serikali ya Kijiji cha Kwemazandu, Nuru Sabuni pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji cha Makorosa, Ramadhan Kijangwa wote kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamejiuzulu nafasi zao kwa nyakati tofauti baada ya kushinikizwa na wananchi kutokana na ubadhirifu wa mali za kijiji.

Ubadhirifu huo uliwekwa hadharani baada ya Mkuu wa Wilaya
ya Korogwe, mkoani Tanga, Bw. Mrisho Gambo, kufanya ziara katika vijiji hivyo hivi karibuni katika Kata ya Magoma.

Wananchi hao walidai kuwa, unadhirifu huo ulihusu mabati 32 ya nyumba ya mwalimu wa Shule ya Msingi Kwemazandu ambayo
yandaiwa kuuzwa.

Baada ya kuwekwa 'kitimoto' kwenye kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC), kabla ya kupigiwa kura ya kutokuwa
na imani naye, Sabuni aliamua kujiuzulu ili kujisafisha.

Akiwa katika mkutano wa hadhara ambao pia ulihudhuriwa na
Bw. Gambo, Sabuni aliwaaga wananchi wake na kudai kuwa,
hakufanya jambo lolote baya katika uongozi wake.

Uamuzi huo uliwafanya baadhi ya wananchi kumshangilia na wengine kwenda kumtunza fedha ili kumpongeza na kumchangua
Bw. Issa Kimesho kuwa Kaimu Mwenyekiti hadi utakapofika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014.

Kwa upande wake, Kijangwa alilazimika kujiuzulu katika
mkutano huo baada ya Bw. Gambo kuunda kamati ambayo
itachunguza uhalali wa Kitongoji cha Mabogo kupandwa
mkonge na Kampuni ya Katani Ltd, kwenye Shamba la
Magoma, wakati wananchi wakidai kuwepo eneo hilo
tangu mwaaka 1970 wakilima na kuchunga.

Kijangwa pia anadaiwa kuuza maeneo ya ardhi mpakani mwa
Wilaya za Korogwe, Handeni na Kijiji cha Kwemazandu, ambapo
wananchi walimchagua Bw. Athuman Shekivuli kuwa Kaimu Mwenyekiti wa kijiji hicho.

No comments:

Post a Comment