07 February 2013

Saba wapitishwa kuwania uongozi TASMA



Na Mwandishi Wetu

WATAALAMU saba wamepitishwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, katika uchaguzi wa Chama cha Wataalamu wa Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA), utakaofanyika Februari 10 mwaka huu jijini Dar es Salaam.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TASMA, Dkt. Paul Marealle, wagombea hao wamepitishwa baada ya kufaulu katika usaili uliofanyika juzi.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Biyondho Ngome, anatetea nafasi hiyo dhidi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Mwanandi Mwankemwa.

Ilieleza nafasi ya Katibu Mkuu ina mgombea mmoja ambaye ni Nassoro Matuzya, wakati nafasi ya Makamu Mwenyekiti haikupata mgombea.

Taarifa hiyo ilieleza, Sheky Mngazija ni mgombea pekee wa nafasi ya Katibu Msaidizi kama ilivyo kwa Juma Mzimbiri, aliyepitishwa kuwania nafasi ya Mhazini. Naye Hemed Mziray ni mgombea pekee wa nafasi ya ujumbe wa Kamati Kuu ya TASMA.

Iliendelea kueleza kuwa nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF imemvutia Joakim Mshanga pekee.

Ilieleza kuwa wapiga kura ni wajumbe sita wa Kamati ya Utendaji na wawakilishi watatu watatu kutoka mikoa ya Geita, Ilala, Iringa, Kagera, Kinondoni, Mtwara, Rukwa, Ruvuma na Temeke. Hivyo jumla ya wapiga kura wote ni 33.

No comments:

Post a Comment