27 February 2013

Mufti Simba amfuta kazi Shekhe Mkuu Morogoro





Na Aziz Msuya, Morogoro

SHEKHE Mkuu na Tanzania, Mufti Issa bin Shaaban Simba, ametengua nafasi ya Shekhe Mkuu mkoani Morogoro, Yahya Semwali akidaiwa kushindwa kusimamia maendeleo ya Waislamu mkoani humo.

Katika barua yake kwa Shekhe Semwali yenye namba MK/BR/UL/03/04/79 ya Februari 19 mwaka huu, Mufti Simba alisema uamuzi huo umefikiwa kwenye kikao cha Baraza la Ulamaa Taifa hivyo anatakiwa kukabidhi ofisi.

Kutokana na uamuzi wa baraza hilo, Mufti Simba amemteua
Shekhe wa Mkoa wa Dodoma, Mustafa Shaaban kukaimu nafasi hiyo kwa barua yenye namba MK/BR/UL/03/04/81 ya Februari 20 mwaka huu na kusisitiza kuwa, nafsi hiyo inapaswa kujazwa ndani
ya siku 90 kwa kufanya uchaguzi mwingine.

“Waumini wa Kiislamu mkoani Morogoro wapewe fursa ya kuchagua Shekhe mwingine wa Mkoa,” ilisema barua hiyo.

Uamuzi huo umepokelewa kwa hisia tofauti na viongozi
mbalimbali wa BAKWATA mkoani humo akiwemo Shekhe
Semwali aliyeondolewa madrakani ambaye alisema madai
yaliyotolewa dhidi yake si sahihi na yameegemea upande
mmoja yakisukumwa na hisia zaidi.


Alisema kuondolewa kwake katika nafasi hiyo kunatokana na
hisia za kuunga mkono msimamo wa Katibu wa Jumuiya na
Taasisi za Kiislamu nchini, Shekhe Issa Ponda jambo ambalo
halina ukweli.

“Hisia nyingine zilizojionesha ni kitendo cha mimi kwenda ibada
ya Hijja kupitia taasisi nyingine tofauti na Baraza la Waislamu nchini (BAKWATA), pamoja na uamuzi wangu wa kutengua uchaguzi wa baraza hili ngazi ya kata, wilayani Gairo.

“Uchaguzi huu ulifanyika kinyime na utaratibu bila ya ngazi
husika kama BAKWATA Wilaya na Mkoa kuwa na taarifa, hili
ndio lililomsukuma Mufti Simba kufikia maamuzi haya japo
baraza hili Mkoa lina taarifa za ukikukwaji husika lakini
bado aliendelea kukaa kimya,” alisema Shekhe Semwali.

Kuhusu madai ya kushindwa kusimamia maendeleo ya Waislamu, Shekhe Semwali alisema hivi sasa katika Wilaya zote kuna miradi ya maendeleo kama ule wa Wilaya ya Ulanga ambako kuna ujenzi wa vyumba vya maduka 14.

Pia kuna mchakato wa upatikanaji ekari 20 kwa ajili ya upandaji
miti ya matunda ambapo hivi sasa walikuwa kwenye hatua za
mwisho kupata ekari nyingine 600.

Alisema Wilaya ya Morogoro Vijijini kuna vyumba vitano vya maduka, Mvomero vyumba vinne vya madrasa na Kilombero
vyumba vitano vya biashara ambapo maendeleo hayo
yametokana na juhudi zake.


Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Baraza la Mashekhe mkoani humo, ambalo lilikaa hivi karibuni kupitia maamuzi hayo, Shekhe Shaaban Nyoni, alisema uamuzi wa Mufti Simba amekiuka Katiba ya BAKWATA.

“Shekhe Semwali alichaguliwa hakuteuliwa hivuyo kama alikuwa
na tatizo, wao kama baraza ndio waliopaswa kuwasilisha tatizo lao
kwa Mufti Simba si vinginevyo.

“Halmashauri ya BAKWATA Mkoa inatarajia kukutana kesho (leo), ili kujadili uamuzi huu na baadaye kikao cha Mashekhe wote wa Wilaya na Mkoa, watakaa kujadili na kutoa msimamo,” alisema.

Kwa upande wake, Imamu wa Msikiti wa Al Aqswaa wa Mazimbu, mkoani humo, Shekhe Mohamed Msoma ambaye ni mjumbe wa Baraza la Mashekhe, alisema si sahihi Mufti Simba kumuondoa
Shekhe Semwali katika nafasi yake.

2 comments:

  1. LABDA PIA ANAHUSISHWA NA TUHUMU ZILIZOPELEKEA RADIO IMANI KUFUNGWA

    ReplyDelete
  2. JAMANI SIMBA KATUMWA AMUONDOE KWA KUWA ANAFANYA MAMBO YA MAENDELEO.SIMNAJUWA WAO HAWATAKI MAENDELEO?NDO MAANA WANAUZA VIWANJA VYA WAISLAM.MOROGORO SIMAMENI SHEIKH YAHYA ASITOKE.

    ReplyDelete