06 February 2013

Mtendaji anusurika kifo akidaiwa kuiba mahindi


Na Masau Bwire, Bunda

OFISA Mtendaji wa Kata ya Iramba, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, Bw. Simon Katikizu, amenusurika kifo baada ya wananchi wenye hasira kumshambulia kwa mawe wakimtuhumu kuiba mahindi ya msaada.

Tukio hilo lilitokea juzi saa 4 asubuhi, Kijiji cha Isanju ambacho
ni Makao Makuu ya kata hiyo ambapo wananchi walikusanyika ili kugawiwa mahindi ya msaada.

Wakati kazi ya kugawa mahindi hayo ikiendelea, wananchi hao walibaini upotevu wa magunia zaidi ya 40 na baada ya kufanya uchunguzi, wakagundua wizi huo ulifanywa na Bw. Katikizu
hivyo walianza kumshambulia kwa mawe na marungu.

“Tumemkamata na mahindi ya msaada akiwa ameyaficha nyumbani kwake, katika Ofisi ya Elimu, kilimo na mengine aliyaweka katika nyumba za rafiki zake, wakati akijaribu kukimbia lilipigwa yowe,” alisema Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM, katika kata
hiyo, Bw. Mohamed Gamba.

Alisema Serikali ilipeleka msaada wa magunia 318 ya mahindi
kwa ajili ya vijiji vitano vya kata hiyo ambapo kila kijiji kilipaswa kupata magunia 63 kutokana na njaa inayowakabili wananchi.

Vijiji vilivyokumbwa na tatizo la njaa ni Isanju, Mugara, Sikiro, Nyarugoma na Mwiruruma, lakini Bw. Katikizu aliiba kiasi kikubwa cha mahindi ambapo kijiji cha Nyarugoma, kiliambulia magunia 26 ndipo wananchi walipokuja juu na kugundua wizi huo.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Joshua Mirumbe, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa, tayari amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri amsimamishe kazi Bw. Katikizu kwa kosa hilo.

“Huyo Ofisa Mtendaji habari zake ninazo, aliwahi kuiba na kuuza mitumbwi 20 iliyokamatwa katika uvuvi haramu hivyo kutokana
na tukio hili, nimeagiza Mkurugenzi amsimamishe kazi kuanzia
leo (jana) na ashitakiwe kwa wizi,” alisema Bw. Mirumbe.

Alisema viongozi wa namna hiyo hawafahi kuendelea kuongoza na wanaitia doa Serikali hivyo hawana budi kuondoka wabaki viongozi waaminifu na waadilifu watakaowaletea wananchi maendeleo.

“Siko tayari kuona viongozi wezi, wabadhilifu na wababaishaji wakiendelea kuwanyonya wananchi kwa kuwaibia, kama wapo wajiondoe kabla sijawafikia, nitaanza na huyo Ofisa Mtendaji
ili iwe mfano kwa wengine,” alisema.

Majira lilipomtafuta Bw. Katikuzu na kumuuliza juu ya tuhuma hizo alidai madai hayo ni uzushi uzushi na hakuna wizi wowote aliofanya bali yeye ni miongoni mwa Watendaji waadilifu wilayani humo wanaoaminiwa kiutendaji na Bw. Mirumbe.

No comments:

Post a Comment