08 February 2013

Moravian kwalipuka, agizo la bodi lapuuzwa



Na Charles Mwakipesile, Mbeya

UONGOZI wa Kanisa la Moravian nchini Jimbo la Kusini, limekataa kutekeleza agizo Bodi ya Dunia ya uongozi wa kanisa hilo kutaka wachungaji 14 waliotimuliwa, warudishwe
kazini na kusisitiza kuwa, bodi hiyo
haina mamlaka hayo.


Msimamo huo umetangazwa jana mjini Mbeya na Mwenyekiti wa jimbo hilo Mchungaji Clement Mwaitebele ambaye alisisitiza kuwa, tayari kanisa hilo limewaondoa wachungaji hao katika utumishi.

Alisema mpango wa uongozi wa dunuia kutaka kuligawa kanisa
hilo nchini, hauwezi kufanikiwa kwani wachungaji husika, wote walifukuzwa kwa mujibu wa Katiba ya jimbo hilo ambao ndio
waliokuwa waajili wao.

Aliongeza kuwa, Makao Makuu ya Jimbo la Kusini yapo Rugwe mkoani Mbeya na ndio waliowasomesha wachungaji hao ndani
na nje ya nchi kutokana na sadaka za waumini hivyo uongozi
wa dunia hauna mamlaka ya kuandika barua ya kusitisha
msimamo wa jimbo lao.

Alionya kuwa, uongozi huo ana uheshimu sana na kama utaendelea kuingilia maamuzi yao na kuleta mpasuko jimboni, atafichua siri
nzito inayoufanya uongozi husika uingilie maamuzi yao ambayo yamezingatia katiba kwa wachungaji waliokiuka kiapo.

“Mimi nawasihi viongozi wa dunia ambao tunashirikiana sana, wajiepushe kuwa sehemu ya mpasuko kwa kuwabeba wachungaji ambao ni watoto wetu sisi si wao vinginevyo utafika wakati tutalipua mambo mazito yaliyojificha.

“Hatutaki tufike huko...jambo la msingi tuheshimiane na tufanye kazi ya Mungu kwa unyenyekevu mkubwa, kanisa hili nchini lina uwezo wa kujiendesha kwa kutegemea sadaka za waumini badala
ya fedha kutoka kwenye bodi zenye masharti na kuwashangilia wachungaji wanaokiuka kiapo na kuleta mipasuko,” alisema.

Mchungaji Mwaitebele alisema, kanisa hilo limekuwa na ushirikiano wa karibu na bodi hiyo lakini barua waliyoandika kutaka maamuzi yaliyotolewa dhidi ya wachungaji hao yasitishwe haiwezekani.

“Naomba niwaambie waandishi wa habari, hatuwezi kubadili msimamo wetu...hawa wachungaji wamefukuzwa, kuondolewa
katika orodha ya wachungaji wa kanisa hili,” alisema.

Aliongeza kuwa, kila Mtanzania aliyesoma anafahamu wazi
kuwa anayestahili kukuwajibisha au kukufukuza baada ya kukiuka makubaliano ni aliyekuajili hivyo wachungaji hao waliajiliwa na Kanisa la Moravian nchini Jimbo la Kusini.

Alisema kikao chenye mamlaka ya kubadili msimamo huo ni Halmashauri Kuu ya Jimbo Mama kinachotarajiwa kukaa Aprili mwaka huu, ambacho kama kitaona umuhimu wa kujadili barua hiyo, itafanya hivyo na kutoa maamuzi lakini kwa sasa uamuzi wa kuwafukuza kazi wachungaji hao uko pale pale.

“Maamuzi mbalimbali ya kanisa hili yanatokana na vikao hivyo kama kutakuwa na uamuzi tofauti na uliotolewa kwa wachungaji
hawa kikao cha Aprili ndio chenye mamlaka hayo.

“Hatuwezi kufanyia kazi barua hii ya bodi ambayo haina mamlaka ya kupinga uamuzi wetu kama jimbo na wakiendelea na msimamo wao tutautangazia umma kuwa wao ndio chanzo cha mgogoro huu,” alisema Mchungaji Mwaitebele.

Aliutaka uongozi wa dunia kuheshimu maamuzi ya jimbo ili kulinda amani, utulivu na kuepusha kutokea mpasuko kwani kufanya hivyo ni kutenda dhambi ambayo wao kama viongozi hawatakuwa tayari kuifanya kutokana na ukweli kuwa, maaamuzi waliyoyachukua yamezingatia taratibu zote.

Alisema wao kama Jimbo Mama la Kusini ndio walioanzisha Uinjilisti katika eneo la Mashariki na baada ya kanisa kukua,
wakapitisha katika Mkutano Mkuu wa Kanisa kulifanya kuwa
Jimbo la Misheni likiwa chini ya uangalizi wao kama ilivyo kwa Jimbo la Mbeya linalolea Jimbo la Misheni Mashariki Arusha na hivyo ni wajibu wao kulilea hadi kufikia Jimbo kamili.

No comments:

Post a Comment