Na Elizabeth Mayemba
KOCHA Mkuu wa zamani wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic baada ya kutemwa na uongozi wa wekundu hao, sasa amefuatilia madai yake baada ya kukatishiwa mkataba wake.
Mara baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara kumalizika, kocha huyo alikwenda kwao Serbia kwa mapumziko lakini uongozi ukawatangazia waandishi wa habari kwamba kocha huyo wamemuacha na hata rudi tena.
Akizungumza na gazeti hili mmoja wa watu wa karibu na kocha huyo, alisema Milovan amefuata chake baada ya kuona uongozi umekaa kimya mpaka sasa huku ukitafuta kocha mwingine hivyo anataka apewe chake ili aendelee na mambo mengine.
"Tangu uongozi wa Simba umuache haujampa taarifa zozote kwamba malipo yake watampa lini, hivyo ameamua kuja mwenyewe ili afuatilie na ikishindikana aende mbele ya sheria ili kupata haki zake kwa kuwa alikuwa bado anamkataba na timu hiyo ya Simba," alisema mtoa habari huyo.
Alisema hata hivyo kocha huyo hana kinyongo chochote baada ya kuachwa, kwani anaamini ni sehemu ya matukio ambayo makocha wengi wanakumbana nayo, hivyo atatafuta timu nyingine ila kwa sasa anafuatilia madeni yake ili arudi kwao.
Awali kulikuwa na uvumi kwamba kocha huyo atarejeshwa kundini, lakini uongozi wa Simba umesema hauna mpango wa kumrejesha kocha huyo na safari yake ya kuja nchini hawaitambui.
Hata hivyo uongozi wa Simba umekiri kwamba kocha huyo anawadai lakini hakuwataarifu kama anakuja kufuatilia madai yake.
Milovan anawadai Simba dola za Kimarekani 24, ambazo ni mishahara ya miezi mitatu kabla ya kutupiwa virago Novemba mwaka jana.
Kocha huyo juzi aliibuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati wa mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Tanzania na Cameroon, ambapo pia alisalimiana na kocha mpya wa Simba aliyerithi mikoba yake Mfaransa Patrick Liewig.
No comments:
Post a Comment