08 February 2013

Majambazi waua,waiba milioni 5





Na Damiano Mkumbo, Singida

WATU watatu wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa katika matukio mawili tofauti yaliyotokea mkoani Singida likiwemo
la mkazi wa Kijiji cha Nkonkilangi, Tarafa ya Shelui, Wilaya
ya Iramba, Gerson Zaphania (35), kupigwa risasi.


Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Linus Sinzumwa, alisema tukio hilo limetokea Februari 5 mwaka
huu, saa mbili usiku wakati marehemu akirejea nyumbani kwake
akitoka matembezini Shelui.

Alisema katika gari hilo lenye namba za usajili T 928 BLK, aina ya Harrier, marehemu alikuwa na mdogo wake Bw. Simon Zephania (25), ambao baada ya kuegesha gari nyumbani kwao, ghafla watu wasiofahamika waliwavamia na kulishambulia gari lao kwa risasi.

“Marehemu alipigwa risasi ya kufuani, mgongoni na kufariki papo hapo, mdogo wake alijeruhiwa mguu wa kushoto...watu hawa pia walimlazimisha huyu kijana agonge mlango wa nyumba ambao ulifunguliwa na Bi. Naomi Zephania (28), ambaye ni mke wa
marehemu na kutaka waoneshwe sehemu zilipotunzwa fedha
na dhahabu wakiwa wamemshikia bunduki.

“Walifanikiwa kupora sh. milloni 5, baadhi ya madini ya dhahabu ambayo thamani yake haijafahamika na kukimbia kusikojulikana,
mdogo wa marehemu amelazwa katika Hospitali ya Wilaya Iramba iliyopo Kiomboi hali yake inaendelea vizuri,” alisema.

Alisema hadi sasa watuhumiwa watano wamekamatwa kuhusiana
na tukio hilo wakiendelea kuhojiwa na watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Hata hivyo, Kamanda Sinzumwa alisema majina ya watuhumiwa hao yanahifadhiwa kutokana na masuala ya kiusalama.

Katika tukio la lingine, wanafunzi wawili wa Shule ya Awali inayoitwa Watembea kwa Miguu, iliyopo Kijiji cha Mnung’una, Tarafa ya Mtinko, wamefariki dunia baada ya kugongwa na gari.

Wanafunzi hao ni Khaliki Ramadhani (7) aliyefariki papo hapo
na Miraji Hamisi (5) aliyefia njiani wakati akipelekwa kwenye Hospitali ya Mkoa Mjini Singida.

Ajali hiyo ilitokea Februari 6 mwaka huu, saa nne asubuhi katika Barabara ya Singida-Nzega ikihusisha gari aina ya Toyota Land Cruiser iliyokuwa likiendeshwa na Bw. Andrew Stephen (48),
mkazi wa Mbezi Luis, Dar es Salaam.

Alisema gari hiyo ambayo ni mali ya Wizara ya Maji Dar es Salaam, ilikuwa ikitokea Singida kwenda Tabora na baada ya kufika eneo la tukio likiwa mwendo kasi, liliwagongwa wanafunzi hao.

Dereva huyo amekamatwa na atafikishwa mahakamani kwa kosa
la kusababisha mauaji ya wanafunzi hao. Alitoa wito kwa madereva wengine kuwa makini wawapo barabarani.


No comments:

Post a Comment