11 February 2013
Milioni 40 kukabiliana na changamoto Ziwa Tanganyika
Na Mwajabu Kigaza, Kigoma
KAIMU Mratibu wa mradi shirikishi wa usimamizi endelevu wa rasilimali za Ziwa Tanganyika Bw. Magesa Bulayi amemkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Bw. Ramadhani Maneno vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 40 ili kukabiliana na changamoto za uharibifu wa Ziwa hilo.
Akikabidhi vifaa hivyo Bw. Bulayi alisema kuwa amechukua uamuzi huwa kutokana na changamoto zinazojitokeza mara kwa mara katika ziwa hilo na vifaa hivyo vitawasaidia watendaji kukabiliana na changamoto ikiwa ni pamoja na uvuvi haramu ambao umekuwa sugu.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na Pikipiki kumi, Komputa, Kamera za digitali, Ptinta pamoja na mashine ya fotokopi ambapo vifaa vitasaidia watendaji wanaoshiriki katika mchakato wa kulinda na kuhifadhi Ziwa hilo ili kufanya kazi zao kwa urahisi na ufanisi ili kufikia malengo.
Watendaji waliokabidhiwa vifaa hivyo ni pamoja na watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma ujiji, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIR).
Akikabidhi vifaa hivyo kwa watendaji mkuu wa wilaya hiyo Bw. Maneno alisema kuwa vifaa hivyo vinatakiwa kutumika kama ambavyo mradi umekusudia na si vinginevyo.
“Kuna ongezeko la vyombo vya uvuvi kutoka vyombo 7,129 kwa mwaka 2006 hadi kufikia vyombo 11,506 mwaka 2011 ambapo ni ongezeko la asilimia 61.4 na kuonekana kuwa asilimia 78 ya vyombo vilivyohesabiwa havikusajiliwa kisheria,” alisema Bw. Maneno.
Hata hivyo Bw. Maneno alisema kuwa mradi unategemea kujenga soko moja katika mwalo wa Kibirizi manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo tathimini ya kumpata mkandarasi imekamilika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment