06 February 2013
Mgogoro Moravian wachukua sura mpya
Na Charles Mwakipesile, Mbeya
MWENYEKITI wa Kanisa la Moravian nchini, Jimbo la Kusini, Mchungaji Clement Mwaitebele, amewataka wachungaji 14 ambao alitangaza kuwafukuza baada ya kukiuka kiapo chao cha utumishi Misheni ya Dar es salaam, kuondoka katika nyumba za kanisa.
Akizungumza na Majira jana, Mchungaji Mwaitebele ambaye alionesha kukerwa na wachungaji hao kuvuruga amani ndani ya
kanisa hilo kwa kujitangazia Halmashauri Kuu yao kinyume na Katiba, alisema uongozi wa kanisa umechukua hatua stahiki kwa watumishi hao kwa kuwa wasaliti katika jimbo mama.
Alisema inashangaza wachungaji hao kudai hawaitambui mamlaka iliyowafukuza badara yake wanasubiri maelekezo ya uongozi wa Bodi ya Dunia (Unity Bord) ulio na Makao Makuu nchini
Ujerumani hali inayoonesha kuwa, pamoja na usomi wao
bado wameshindwa kutambua taratibu.
“Kwa kuwa wameonesha kiburi cha kutoitambua mamlaka yangu kikatiba, natangaza rasmi kuwa kuanzia leo (jana), nimefuta ujio
wa Bodi ya Dunia kuja nchini kuzungumzia tatizo hili kwa sababu
tayari limekwisha hawana umuhimu wa kuja,” alisema.
Mchungaji Mwaitebele alisema Ofisi la Dunia ni Makao Makuu
ya Jumuia ya kanisa hilo kama ilivyo Umoja wa Mataifa ambao hauwezi kuingilia mambo ya ndani nchini Tanzania hadi
unapopewa taarifa na uongozi wa nchi.
“Sisi kama viongozi wa jimbo mama, hatuoni umuhimu wa hawa viongozi Bodi ya Dunia kuja kusikiliza mazungumzo kwa sababu tayari tumemaliza mgogoro uliokuwepo na taratibu za kisheria zinachukuliwa,” alisema.
Aliwataka wachungaji hao kuhama mara moja katika nyumba za kanisa kwani hivi sasa si watumishi tena wa kanisa hilo kwa mujibu wa katiba baada ya kushindwa kulinda kiapo chao kilichowataka kuwa watii uongozi badala yake wanatumika kuleta mipasuko.
Aliongeza kuwa, wao walifuata utaratibu wa kanisa wa kukaa mezani ili kusikiliza matatizo ya Misheni hiyo baada ya Sinodi
ya eneo hilo kumuondoa madarakani aliyekuwa Mwenyekiti wao.
“Wakati mazungumzo yakiendelea, Mwenyekiti huyo alitangza Halmashauri Kuu yake jambo lililoonesha wazi usaliti mkubwa katika kanisa,” alisema Mchungaji Mwaitebele.
Aliwaonya Watunza Hazina wa kanisa hilo kuepuka kushirikiana
na wachungaji hao kwa kuchukua fedha za matumizi yao binafsi kwani uongozi wake utawaburuta mahakamani kwa kosa la wizi
wa fedha za umma jambo ambalo asingependa litokee.
Alisema Mamlaka iliyowafukuza wachungaji hao ni halali ambayo ilichaguliwa na Mkutano Mkuu wa Kanisa na hivyo madai kuwa walipaswa kufukuzwa kwa pendekezo la Askofu ni upotoshaji wa wanaoufanya ili kuliyumbisha kanisa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment