01 February 2013

Meru yazipa 'tafu' timu sita


Na Queen Lema, Meru

WILAYA ya Meru, imetoa sh. milioni 8 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali vya michezo kwa timu sita za wilaya hiyo, lengo likiwa kuendeleza vipaji vya michezo ndani ya wilaya hiyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi wilayani hapa jana Mkuu wa wilaya hiyo, Munasa Nyirembe alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kuona kuwa kuna umuhimu wa wilaya yake kuhakikisha inaendeleza vipaji.

Munasa alisema fedha hizo zilitolewa na wilaya hiyo kwa kuwa imegundulika wachezaji wengi, hasa wa soka ambao wana vipaji lakini tatizo linaonekana ukosekanaji wa vifaa vya michezo.

Alisema fedha hizo zitaweza kunufaisha timu sita za wilaya hiyo, ambapo timu zao zitaweza kushiriki mashindano ya Kombe la CCM Wilaya ya Meru, ambayo yameanza na yanatarajiwa kumalizika Februari 5, mwaka huu.

“Tunaona Meru ni moja ya wilaya ambazo zina vipaji vingi, lakini kitu kimoja ni kuwa bado wachezaji wetu wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa vifaa, tumeona kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha tunawapa watu hawa fursa ya kuendelea kufanya vizuri zaidi," alisema Munasa.

Pia alisema mbali na kuwapa vifaa vya hivyo timu sita za wilaya hiyo, lakini pia wilaya hiyo imejipanga kuhakikisha wanapanga, ili kuandaa mechi za kirafiki ambazo zitasaidia kuibua vipaji zaidi.

Naye Ofisa Utamaduni wilaya hiyo, Senyaeli Palangyo alisema wamejipanga kuendelea zaidi katika michezo mbalimbali kwa kuwa vipaji vingi, vinaweza kuendelezwa ingawa awali hapakuwa na hamasa za kutosha.

No comments:

Post a Comment