05 February 2013

Mabanda 19 yateketea kwa moto Mwenge



Na Peter Mwenda

MABANDA 19 ya vipodozi, viatu na nguo za mitumba yaliyopo katika Stendi ya Mabasi daladala iliyopo Mwenge, Dar es Salaam, yameteketea kwa moto na kusababisha hasara kwa wamiliki wake.

Baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wakimiliki mabanda hayo, walijikuta wakibubujikwa machozi na kutoamini kilichotokea kutokana na mali zao kuteketea kwa moto na nyingine kuibwa
na vibaka waliokuwa eneo la tukio.

Wakizunguza na Majira, mashuhuda wa tukio hilo walisema moto huo ulianza saa nne asubuhi katika banda moja na kusambaa kwenye mabanda mengine ambapo jitihada za kuuzima, zilianza saa 5:30 baada ya kuwasili gari la zima moto.

Kamanda wa Kanda Maalum ya Zimamoto na Uokoaji Dar es Salaam, Bakari Mrisho, alisema uchunguzi wa moto huo na ule uliotokea jengo la PPF Tower, utafanyika na majibu kutolewa.

Wakati huo huo, hali ya huduma katika jengo hilo ambalo juzi lilinusurika kuungua moto katika ghorofa ya 18, zitanza kutolewa baada ya mafundi kukagua mfumo wa umeme.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa PPF, Bw. William Erio, alisema kinachoendelea katika jengo hilo kwa sasa ni kukausha maji
katika nyaya ili kurudisha umeme ili wapangaji wao waweze
kuendelea na kazi kama ilivyokuwa awali.

“Timu ya wataalamu inaendelea kufanya uchunguzi wa moto
katika chumba cha mawasiliano ambako ndio ulianzia, kazi ya kwanza ni kukausha maji ili kurudisha umeme,” alisema.

Alisema katika tukui hilo , hakuna hasara iliyotokea au kusababisha madhara kwa mtu bali chumba kilichoungua ni kile cha mawasiliano pekee.

No comments:

Post a Comment