21 February 2013

JKT watakiwa kutumia karate vizuri


Na John Gagarini, Kibaha

VIJANA wanaohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), wametakiwa kuutumia mchezo wa karate kama silaha ya kupambana na maadui wa nchi na si kwa watu wema.

Hayo yalisemwa juzi na Mkurugenzi wa SUMA JKT, Jenerali Mwamakala Killo wakati akifunga mafunzo ya awali ya kijeshi kwa vijana, yaliyopewa jina la Operesheni Sensa kwenye kambi ya JKT ya Ruvu wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Jenerali Killo alisema mafunzo ya mchezo huo ni sawa na silaha, ambayo mtu anatembea nayo hivyo lazima aitumie kupambana na adui na si kupambana na ndugu zake.

“Mchezo wa karate ni silaha, kwani inaua na ina jeruhi hivyo kikubwa lazima kuwe na nidhamu, pia mchezo huu unakupa ukakamavu na nidhamu na endapo utatumiwa vibaya, unaweza kuwadhuru wengine hivyo utumiwe kupambana na adui wa nchi,” alisema Jenerali Killo.

Alisema vijana wa Tanzania, wanatakiwa kuenzi tamaduni za hapa nchini na kuachana na za nje, kwani utamaduni wa nje ambao hauenzi wa kwetu ambao ni mzuri.

“Vijana wameonesha michezo mbalimbali, ambayo inakuza utamaduni wa Kitanzania amabo una heshima tofauti na wa nje, ambao unawaharibu vijana hivyo JKT inaweza kukuza utamaduni wetu na kuutangaza kwa mataifa ya nje,” alisema.

Alisema michezo kama ya kucheza na nyoka na ngoma za makabila mbalimbali ni moja ya tamaduni, ambazo zinapaswa kuendelezwa ili kulinda utamaduni wa nchi, kwani unawavutia watu hata wa mataifa ya nje.

Aliwataka vijana waliohitimu mafunzo hayo kuendeleza vipaji vyao, kwani vitawafanya kujiongezea kipato pia kupata ajira, ambapo baadhi yao wameajiriwa kupitia michezo mbalimbali hapa nchini.

No comments:

Post a Comment