05 February 2013

Jengo la PPF Tower lanusurika kuungua




Na Rehema Maigala

JENGO la PPF Tower, lililopo Mtaa wa Ohio, jijini Dar es Salaam, jana lilinusurika kuungua baada ya moto kuzuka ghafla kwenye ghorofa ya 18.


Moto huo ulianza saa 12:45 asubuhi na kufanikiwa kuzimwa saa tatu asubuhi na vikosi mbalimbali zima moto. Vikosi hivyo ni Bandari,
Kikosi cha Zima Moto na Uokoaji pamoja na Knight Support.

Kazi ya kuzima moto huo ilianza saa moja asubuhi baada ya Mkurugenzi Mkuu wa PPF, Bw. William Erio, kupiga simu
katika vikosi mbalimbali vya zima moto na uokoaji.

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Saidi Meck Sadiki, alisema ujenzi wa jengo hilo umezingatia masharti ya kuzuia ajali za moto.

“Niupongeze uongozi wa PPT Tower kwa kuzingatia vigezo ndio maana moto huu haukuweza kufika kwenye ofisi mbalimbali baada ya kudhibitiwa mapema, natoa wito kwa majengo mengine yote kuzingatia vigezo na masharti wanayopewa,” alisema Bw. Sadiki
na kupongeza miundombinu ya jengo hilo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema jeshi hilo linaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha moto huo.

Kaimu Kamishna Jenerali wa Kikosi cha Zima Moto na Uokoaji, Bw. Pius Nyambacha, alisema vikosi vyote vilivyoshiriki kuuzima moto huo, vimefanya kazi hiyo kwa ushirikiano mkubwa.

Alisema hivi sasa wapo katika mchakato wa kukagua majengo
yote marefu na lile ambalo litakutwa halina vifaa vya kuzuia ajali
za moto litafungwa hadi watakapotimiza masharti.

No comments:

Post a Comment