06 February 2013

Hukumu ya vigogo Shirika la VUKA kutolewa Machi 11


Na Rehema  Mohamed

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaaam, Machi
11 mwaka huu, inatarajia kutoa hukumu ya kesi ya wizi wa zaidi
ya sh. milioni 100, inayowakabili vigogo wa Shirika la VUKA-Tanzania, linalohusika kuendesha miradi ya UKIMWI.

Washtakiwa hao ni Mwenyekiti wa shirika hilo Bw. Adolf Mrema, Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Utawala, Bi. Hilda Urassa pamoja na mshauri Bw. Straton Simon, ambao wanadaiwa kutumia fedha
za miradi ya UKIMWI.

Jana kesi hiyo ililetwa mahakamani hapo kwa ajili ya utetezi ambapo washtakiwa hao, walijitetea mbele ya Hakimu Sundi
Fimbo na kufunga ushahidi wao.

Wakitoa utetezi wao, washtakiwa hao walikana kutumia isivyo
halali fedha hizo kutoka Shirika la Maendeleo la Denmark (DANIDA) na Shirika la SAT-Tanzania.

Kwa nyakati tofauti, washtakiwa hao walidai fedha hizo walizitumia kwa ajili ya matumizi ya ofisi kama dawa kwa ajili ya waathirika wa VVU, kuendesha semina na kulipa mishahara ya wafanyakazi wao.

Hata hivyo, washtakiwa hao hawakuwa na nyaraka za kuthibitisha matumizi ya fedha hizo na kudai kuwa, nyaraka hizo zilichomwa moto na mwenye nyumba aliyewapangisha ofisi kwa kuwa waliifunga.

Walidai mwenye nyumba baada ya kuona wamefunga osifi, aliamua kumpangisha mtu mwingine hivyo kutoa vitu vyao na kusababisha nyaraka zao kupotea na nyingine kuchomwa moto kama uchafu.

Katika kesi hiyo, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka
37 likiwemo la kugushi, wizi na matumizi mabaya ya fedha.

Inadaiwa kuwa, washtakiwa hao walitenda makosa hayo kati
ya Juni11,2006 hadi Desemba 2007, Temeke, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment