11 February 2013

Bodi yaibua mapya sakata la Moravian


Na Charles Mwakipesile, Mbeya

BODI ya Kanisa la Moravian Duniani, imekana kuwakumbatia wachungaji 14 wa kanisa hilo Misheni ya Dar es Salaam na
Zanzibar waliofukuzwa kwa madai ya kuasi kiapo chao.

Akizungumza na gazeti hili jijini Mbeya jana, Makamu Mwenyekiti wa bodi hiyo, Mchungaji Nosigwe Buya, alisema kilichofanywa na bodi ni kusuluhisha mgogoro uliopo bila kupendelea upande wowote.

Alisema bodi hiyo ilimteua kusuluhisha mgogoro huo kutokana
na athari zake kwa umoja wa kanisa hilo ambalo kwa muda mrefu limekuwa na amani hivyo kuwa mfano wa kuigwa.

Aliongeza kuwa, wakati akitafuta suluhi ya mgogoro huo, alifuata taratibu zote za kuhakikisha amani inapatikana ili kazi ya Mungu iendelee kutolewa lakini alipata vikwazo vya kukosa ushirikiano katika baadhi ya maeneo.

“Vikwazo hivi vilinifanya nishindwe kumalizia hatua ya mwisho
ya kuzikutanisha pande mbili zinazovutana, kimsingi mvutano huo umekolezwa na kila upande kuonekana una haki.

“Hali hii ilinifanya nishindwe kuutatua kutokana na baadhi ya maamuzi kuamuliwa bila ya mimi kuwepo hivyo kukosa neno
la kusema zaidi ya kutoa taarifa za nilipofikia lakini nikipata
nafasi nitakutana na viongozi wa kanisa hili nchini (KMT),”
alisema Mchungaji Buya.

Alisema yeye ni Mchungaji mwenye uchungu na anapoona amani inapotea, hawezi kushangilia waala hafurahishwa kuona kanisa likifungwa na kusababisha waumini wakose ibada kwa sababu
kuna watu wamekwenda mahakamani.

“Jambo hili si sawa na mimi kama msuluhishi, sina masilahi na upande wowote, Bodi ya Dunia ni Ofisi ya Umoja na jukumu lake
ni kulinda umoja katika kanisa, haiko kwa ajili ya kuchochea migogoro na kulilinda kundi linalokiuka taratibu,” alisema.

Mchungaji Buya ambaye pia ni Mwenyekiti wa kanisa hilo Jimbo
la Kusini Magharibi na Mwenyekiti wa Afrika, alisema kamwe uongozi wa Dunia hauwezi kufanya kazi ya kuvuruga majimbo.

Alisema wao wanaunga mkono taratibu zote zinazolenga kulindwa na kuheshimiwa kwa katiba ya kanisa hilo katika jimbo husika na kukanusha madai ya kuahidi kuwapatia jimbo lingine wachungaji waliofukuzwa Misheni ya Dar es Salaam.

“Hatuwezi kuahidi kuahidi kuwapa jimbo wachungaji wa Dar es Salaam ili wajitenge na Jimbo la Kusini badala yake tutaungaana
nao kuhakikisha amani na utulivu vinakuwepo jimboni,” alisema.

Aliongeza kuwa, uongozi wa Dunia na Afrika utaendelea kushirikiana na uongozi wa Jimbo la Kusini kila inapohitajika
ili kulinda umoja uliopo katika kanisa hilo ambalo linahimiza
upendo na kuhakikisha waumini wanamwabudu Mungu katika
roho na kweli ili kuondokana na vurugu zilizopo.

Mwenyekiti Buya alionya suala zima la mipasuko katika kanisa
hilo ambayo inapoteza mwelekeo wa waumini hasa katika kipindi hiki chenye changamoto nyingi za kuhakikisha jamii ya Watanzania inakuwa na maadili mema na kulinda maadili ya Ukrisro.

Aliwataka wachungaji wanaodaiwa kuasi taratibu za kanisa Jimbo
la Kusini na kufukuzwa utumishi, kutulia na kutumia hekima ili kupata utatuzi wa jambo hilo badala ya kuendeleza malumbano
ambayo hayaleti sifa kwa Mungu.

No comments:

Post a Comment