21 January 2013

Wawili watakiwa kuachia ngazi bodi ya filamu


Na Amina Athumani

KATIBU Mtendaji wa Bodi ya filamu Tanzania aliyechaguliwa na Serikali, Joyce Fisoo na Ofisa wa COSOTA, Yustus Mkinga wametakiwa kuachia nyadhifa zao kwa madai kuwa utendaji wao si mzuri.

Endapo watashindwa kufanya hivyo ndani ya kipindi kifupi Chama cha Waigizaji wa filamu Tanzania (TDFAA), kitaitisha maandamano ya wasanii nchi nzima na yatafanyika mfululizo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, katika kikao cha kuadhimia kuwang'oa viongozi hao kilichoandaliwa na TDFAA, Mwenyekiti wa TDFAA, Michael Sangu alisema wao kama wasimamizi wa wasanii hawana imani na COSOTA pamoja na bodi hiyo kupitia viongozi wao Mkinga pamoja na Joyce.

Alisema wao wanamshukuru sana Rais Kikwete kwa jitihada zake za kuongeza ajira kwa vijana, hivyo wangependa kuona mamlaka za sanaa nchini zihusishe pia wasanii miongoni mwa watendaji wake ili kuelewa kinachoendelea katika tasnia ya filamu.

"Hii haikubaliki, na ndio msingi wa malalamiko yetu, Ofisi ya bodi haitoi ushirikiano kabisa katika hoja zetu, mtazamo wa kiongozi mtendaji ni kuvuna pesa tu,"alisema Sangu na kuongeza kuwa.

"Katika hali ya kusikitisha kwa nyakati tofauti ikiwemo katika msiba wa msanii mwenzetu, Juma Kilowoko 'Sajuki', Katibu Joyce amekuwa akiwaambia baadhi ya wasanii kwamba 'mnajisumbua hakutakuwa na mabadiliko yoyote ya gharama katika kanuni za filamu, hivyo msihangaike',"alisema.

Alidai Joyce amekuwa mmoja wa watendaji wa Serikali wasiowatakia mapenzi mema wasanii na kwamba ushahidi upo wa kutosha ikiwemo katika vikao kadhaa mtendaji huyo amekuwa akiwakashifu wasanii.

"Hatumuhitaji kwenye bodi na akiendelea kuwepo hatutampa ushirikiano wowote na tunamuomba waziri (Waziri wa Habari Vijana, Utamaduni na Michezo, Fenella Mkangara) azingatie hili kwa maslahi ya tasnia ya filamu nchini,"alisema Sangu.

Alisema Kwa upande wa Mkinga wa COSOTA amekuwa akishirikiana na wezi  wa kazi za wasanii na ndio maana wamekuwa hawaiogopi COSOTA kwa kuwa ni marafiki wa Mkinga.

Kutokana na hali hiyo Sangu alisema hawataweza kwenda katika urasimishaji wa kutumia kanuni hizo ambazo baadhi ya vipengele vyake vipo kwa ajili ya kumkandamiza msanii na muandaaji wa filam kinyume na lengo la urasimishaji.

No comments:

Post a Comment