28 January 2013

Waushutumu NASA kuficha sayari tishio


Na Danny Matiko

KATIKA toleo lililopita tulishia kuona baadhi ya wananchi wa Marekani wakilishutumu shirika la anga za juu la nchi hiyo, NASA, wakidai kuwa limekuwa na tabia ya kuficha masuala mengi ambayo ni matokeo ya uchunguzi wa anga za juu
.

  Wananchi hao wakereketwa wa masuala ya anga wamekuwa wakitumia mitandao ya mawasiliano ya kijamii kuelezea wasiwasi wao kwamba mwenendo huo (wa NASA) kuficha matokeo ya ugunduzi katika masuala ya anga, ndio maana hata taarifa rasmi za uwepo wa sayari tishio kwa dunia, maarufu kwa jina la "Nibiru", zimefanywa kuwa siri kubwa.

  Baadhi ya wananchi hao pia wamekuwa wakidai kuwa hata mavazi waliyovaa wanaanga wa nchi hiyo katika safari zao za kwenda kutua mwezini, yalikuwa yamewekewa mionzi hatari ya nyuklia ili kuwawezesha wanaanga hao kujihami dhidi ya kiumbe chochote ambacho kingejaribu kuwavamia ama wakati chombo chao kikiwa njiani huko anga za juu au wanaanga hao wakiwa tayari wametua mwezini.

  Wananchi hao wamekuwa wakiishutumu NASA kwa kukanusha vikali uvumi huo wakati, wanasema, ni kweli tupu.

  Wanadai kuwa vitufe vya kufyatulia mionzi hiyo huonekana dhahiri upande wa kifuani mwa kila mmoja wa mwanaanga hao.

  Hata hivyo, NASA wamekuwa wakikanusha kila mara madai hayo na kueleza kuwa vitufe hivyo ambavyo kwa kawaida huonekana kwenye mavazi ya wanaanga huwa na kazi nyingi, ikiwemo kuwezesha kusikika mawasiliano miongoni mwao na pia kuchukuwa vipimo vya kiafya kwa kila mwanaanga husika.

  Mathalani, wakati wa maadhimisho ya miaka 42 tangu binadamu wa kwanza alipotua mwezini Julai 20, 1969, Makala haya tulifuatilia madai hayo, ambapo licha ya kukanushwa vikali kwa simu na msemaji wa NASA, pia tulifuatilia kwa njia ya mtandao ili kuona ulivyokuwa uundwaji mavazi hayo.

  Tuliwaletea wasomaji wetu jinsi mavazi hayo yalivyotengezwa, ambapo pia tuliweza kufuatilia mpaka kwenye kiwanda kilichoyatengeneza na kuona fomyula iliyotumika kuyasuka.

  Mavazi hayo ni kofia nene yenye miwani ambayo pia hufanyakazi kama kamera, simu na kinasa sauti ambavyo vilifungamanishwa na kofia hiyo kwa ndani, suruali iliyounganishwa na koti lake ambavyo kwa pamoja vimefungamanishwa na viatu mfano wa buti.

  Kadhalika, tulibaini kuwa vitufe vinavyoonekana upande wa vifuani hutumika kuunganisha waya za kupitisha mawimbi ya umeme kutoka kwa mwananga akiwa ndani ya chombo cha anga na kuunganishwa na mtambo maalumu ambapo kwa kutumia mbinu hiyo hutuma vipimo vya afya yake moja kwa moja mpaka duniani.

  Hiyo huwezesha wanasayansi kufuatilia mabadiliko yoyote ambayo yangeweza kujitokeza katika mwili wa mwaanga husika, na hivyo pia, kuwezesha wataalamu wa anga kujifunza ni wakati gani au katika mazingira gani mwanaanga aweza kukutwa na tatizo la kiafya awapo huko anga za juu.

  Ikumbukwe kuwa NASA ndiyo hubeba jukumu na dhamana ya usalama wa wanaanga hao, ingawa pia huwa kuna vyombo vingine kama vile bima, na kadhalika.

  Mavazi hayo pia kwa ndani yaliwekewa sponji nene isiyopitisha maji, joto, wala ubaridi visivyotakiwa, ambapo pia upande wa mgongoni mavazi yaliunganishwa na mtungi wenye hewa ya oksijeni kwa ajili ya mwanaanga kupumua.

  Hiyo ni kwa kuwa hewa iliyopo huko anga za juu ina sumu, na hivyo kutofaa kwa matumizi ya binadamu.

  Mavazi hayo rasmi sana kwa usalama wa wanaanga wa mwezini yalikuwa na uzito wa kilo 80 hapa duniani, lakini kule mwezini uzito huo ulipungua mpaka kuwa kilo 3.

  Hivyo basi, tulifuatilia mpaka siku mavazi hayo yalipochukuliwa kutoka kiwandani na kupelekwa makao makuu ya NASA, ambapo jozi 3 za mavazi hazo zilikabidhiwa kwa mtunzaji wa stoo na kuhifadhiwa kwenye chumba maalumu.

  Tulifuatilia mpaka siku mavazi hayo yalipoondolewa hapo stoo usiku wa kuamkia safari ya Apollo ya kwanza kwenda mwezini, ambapo yalipelekwa kwenye chumba kilichotumika kuwaaga wanaanga hao watatu tayari kwa safari.

  Kwa kuwa Apollo iliondoka saa 3:32 asubuhi, wanaanga walianza kujiandaa kuanzia saa 10 alfajiri, ambapo mojawapo ya majukumu ilikuwa ni pamoja na kuyavaa mavazi hayo kwa mara ya kwanza mbele ya kandamnasi ya viongozi wa NASA ili kuona kama wangeweza kuyavaa wakiwa peke yao muda mfupi kabla ya chombo kuanza kutua mwezini.

  Baada ya hapo wanaanga hao waliyavua mavazi hayo, ambapo wahudumu waliyabeba na kuyaingiza ndani ya Apollo ambayo ilikuwa tayari imeegeshwa mahali pa kuanzia safari.

  Katika hatua zote hizo za kushughulikia mavazi hayo, haikuoneshwa mahali popote kama yaliongezewa nakshi au kinga nyingine, au hata kuwekewa mionzi hatari ya kinyuklia.

  NASA walidai kuwa wachunguzi wao wa anga walikwishabaini kutokuwepo hatari yoyote huko mwezini, na hivyo hawakuwa na sababu ya kuwahami wanaanga hao kwa kutumia nyuklia.

  Ilidaiwa kuwa tishio pekee la usalama wa Apollo hiyo ya kwanza kwenda huko mwezini ilikuwa ni kutoka kwa chombo cha anga kisichojulikana, maarufu kama UFO, ambacho kilijitokeza siku ya 3 Apollo ikiwa safarini huko anga za juu.

  Mwanaanga Michael Collins ambaye alikuwa rubani wa Apollo hiyo, anadai kwenye kitabu chake cha "Carrying the Fire" (kubeba moto) kwamba UFO hiyo ilijitokeza ghafla kutoka kusikojulikana na kumudu kwenda sambamba na mwendo mkali wa Apollo kwa masafa marefu.

  Wakati huo Apollo ilikuwa katika kasi ijulikanayo kama "transonic speed", ambayo ni takribani kilometa 40,000 kwa saa ( sawa na kilometa 11 kwa sekunde).

  Anaeleza kuwa walipotoa taarifa duniani kwa makao makuu ya NASA kwamba kulikuwa na chombo kigeni kinawafuatilia, walijibiwa kuwa "hiyo ni UFO, achana nayo, zingatieni safari maana ndiyo muhimu kwenu." Baadaye UFO hiyo ilitoweka kama ilivyokuja.

  Kadhalika, shutuma nyingine dhidi ya NASA ni madai kwamba inaficha habari za UFO, vyombo ambavyo asili yake imebaki kuwa kama kitendawili katika sayansi ya anga.

  NASA wamekuwa wakidai kuwa hawafahamu chanzo cha kuwepo UFO hizo, na pia kwamba hawahusiki katika uundwaji wake.

  Raia hao wa Marekani hudai kuwa NASA wanafahamu ukweli kuhusiana na UFO hizo, kwani ni vyombo kutoka anga za juu ambazo wao NASA wanazichunguza.

  Katika shutuma za hivi karibuni, hususan kufuatia madai ya viongozi wa baadhi ya dini huko Marekani kwamba mwaka jana 2012 ungekuwa ndio mwisho wa dunia, NASA wanabebeshwa shutuma kwamba wanaficha habari za ujio wa sayari ya "Nibiru" ambayo eti ilitarajiwa kuja kuigonga dunia na kuisambaratisha.

  Baadhi ya raia wa Marekani wanadai kuwa uwepo wa sayari hiyo unafichwa kwa makusudi fulani yenye maslahi kwa Mataifa Makubwa ambayo, inadaiwa, wakuu wa shirika hilo ni kama wakala wao.

  Raia hao wanadai kuwa sayari hiyo ni tishio kwa dunia, kwani hata zama za kale ujio wake uliwahi kusababisha madhara makubwa kwa dunia, ikiwemo ile "Gharika ya Nuhu."

  "Nibiru" ambalo ni jina lenye asili ya lugha mojawapo za kale nchini Irak, ambapo tafsiri yake sahihi kwa Kiswahili ni sayari "ipitayo" karibu na anga ya dunia.

  Wasomaji wetu, kutokana na utata uliopo duniani kuhusu kuwepo au kutokuwepo sayari hiyo ya "Nibiru," tutawaletea habari zake kamili na sahihi kupitia mfululizo wa Makala yajayo.

  Hivyo basi, usikose habari za sayari hiyo ambayo inayodaiwa kuwa kwa sasa ipo huko anga za mbali, na inaendelea kusogea taratibu ili hatimaye iweze kuingia katika eneo la anga linalotumiwa na sayari za hili jua "letu.

No comments:

Post a Comment