28 January 2013

Sera ya utunzaji mazingira iwe endelevu



Na Jovin Mihambi.

SERIKALI kupitia Ofisi ya Rais kitengo cha mazingira imeweka bayana kwamba kila jamii hapa nchini iweze kutunza na kuhifadhi mazingira ili kurudisha mandhari ya mazingira kama yalivyokuwa kabla ya nchi ya Tanganyika kupata uhuru wake miaka 51 iliyopita.


Kutokana na sera hiyo, kizazi cha sasa kama kwa kufuatia historia ya hapo nyuma, hakiwezi kukubaliana kwamba katika Ziwa Victoria kulikuwa na viumbe hali kama vile samaki wa aina mbali mbali ambao hadi sasa baadhi yake wametoweka kabisa.

Tukichukulia mfano katika Ziwa Victoria, hapo miaka ya nyuma kabla ziwa hilo halijaingiwa na masuala ya ujangili, kulikuwa na aina mbali mbali ya samaki ambazo kwa sasa tayari ni nadra kupatikana au pengine zimetoweka kabisa.

Samaki ambazo tayari zimepotea kabisa katika ziwa Victoria kwa upande wa Tanzania ni pamoja na sangara, fulu, muru sire, sulubab na sato pamoja na aina nyingi za samaki kwa kuzitaja chache tu na kama zikipatikana na kuvuliwa katika ziwa hilo, kuna baadhi ya kizazi cha sasa cha vijana wetu hawawezi kula pengine watadai kuwa viumbe hao ni jamii ya nyoka na kwamba hawaliwi kabisa.

Lakini kwa upande wa nchi ya utafiti ambao umefanywa na taasisi ya utafiti ya Kenya Marine Research Institute unaonyesha kuwa samaki kama vile fulu, muru, sire, sulubab na samaki wengine tayari wameanza kuongezeka katika Ziwa Victoria upande wa Kenya kutokana na wananchi katika nchi hiyo kutunza na kuhifadhi mazingira ya Ziwa Victoria.

Pia utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na taasisi ya Taifa nchini Uganda ya National Fisheries Resource Research Institute (NaFIRRI) unaonyesha kuwa samaki aina ya fulu ambayo kwa lugha ya Kiganda inajulikana kwa jina na “enkejje” ambayo miaka ya sabini ilikuwa ikivuliwa kwa kuchagia kiasi cha asilimia 70 kwa idadi yote ya samaki zote zilizovuliwa miaka ya 1970 lakini hadi miaka ya 1980 uvuvi wa samaki aina ulikuwa chini ya kiwango cha  asilimia kumi.

Naye Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa Serikali ya Misri Profesa Dkt. Mohamed Bahaa El-Din Ahmed, anasema kuwa Ziwa Victoria lina umuhimu mkubwa kwa nchi zinazopata huduma kutoka ziwa hilo pamoja na nchi ya Misri ambayo inapata huduma ya maji hayo kupitia mto Nile.

Anasema kuwa katika miaka ya sitini na sabini, Tanzania ilikuwa moja ya nchi za Bonde la mto Nile zlizoshiriki kwenye mradi wa ukusanyaji wa takwimu za maji ambao ulijulikana kama Lake Victoria Hydrometric Project

Na kusema kuwa umuhimu wa Watanzania kutunza na kulinda mazingira ya Ziwa Victoria sio kwa manufaa ya nchi ya Tanzania pekee bali pia kwa manufaa ya nchi ya Misri ambayo inategemea maji kutoka Ziwa Victoria.

Anasema kuwa nchi ya Misri inanufaika kwa kiasi kikubwa katika kilimo cha umwagiliaji pamoja na shughuli zingine ambazo zinatokana na maji ambayo yanapitia mto Nile hadi Misri na shughuli hizo zinaweza zikakwamishwa endapo Watanzania hawatajikita katika kutunza na kuhifadhi mazingira ya Ziwa Victoria.

Aidha, tafiti mbali mbali ambazo zimefanywa na wataalamu wa masuala ya mazingira ya Ziwa Victoria pamoja na Bonde la Maji Kanda ya Ziwa, zinaonyesha kuwa mazalio ya samaki katika mabonde ya mito ambayo hutiririsha maji katika Ziwa Victoria nayo yamehadhiriwa vibaya na baadhi ya watu ambao hulima kando kando ya mito, kufanya shughuli za ufugaji pamoja na shughuli zingine ambazo ni athari kubwa kwa viumbe hai ambao hupatikana katika mito na maziwa.

Mratibu wa LVEMP 11, Bw Pius Mabuba anasema kwamba taasisi yake tayari imejikita katika kutatua tatizo la uchafuzi wa mazingira katika Ziwa Victoria ambao unatokana na uchafu na uharibifu wa mazingira kutoka Mto Simiyu na Duma iliyoko katika mkoa wa Simiyu.

Anasema kwamba vikundi vya kijamii vimeanzishwa kwa ajili ya kunusuru uchafuzi wa mazingira ya mito hiyo na kusema kuwa vikundi hivyo pia vitasaidia katika kuinua kipato kwa wananchi na kujiongezea uchumi katika jamii.

Vikundi hivyo vitajihusisha na upandaji miti, ujenzi wa mabwawa ya kunyweshea mifugo, kilimo ambacho ni endelevu pamoja na shughuli zingine na kuongeza kuwa katika miradi hiyo, tayari serikali kwa kushirikiana na wahisani kutoka nje imetenga sh.bilion 1,825,000,000.00 kwa ajili ya shughuli hiyo.

Anasema kuwa kamati mbali mbali ambazo zitasimamisha shughuli za utunzaji na uhifadhi mazingira ya mto Simiyu na Duma tayari zimeundwa na mikataba kati ya halmashauri husika mkoani Simiyu ambazo zitasimamia miradi hiyo imekwishasainiwa tangu Desemba 20, mwaka jana.

Naye Bw Lawrence Kalabegile ambaye pia ni mmoja wa wadau wakuu katika Mradi wa Hifadhi Mazingira ambaye katika kikao cha wenyeviti na wajumbe wa kamati za mradi wa LVEMP 11 wakati wa kikao ambacho kimefanyika katika hoteli ya JB Belmont jijini Mwanza kuanzia Januari 7 hadi 9,

Anasema kwamba licha ya taasisi ya LVEMP 11 kujikita katika kusimamia shughuli za kulinda na kutunza mazingira ya Ziwa Victoria, jamii pia inao umuhimu mkubwa juu ya kujikita zaidi katika upandaji miti ili kurudisha mandhari ya nchi kama ilivyokuwa miaka hamsini iliyopita.

Anasema kuwa anaonelea hivyo kutokana na nchi ya Tanzania ambayo awali ilikuwa nchi ya “Kijani” sasa imebadirika kuwa nchi ya jangwa.

Anasema kwamba vijana wa Kitanzania wa sasa wakielezwa kuwa mkoa wa Mwanza pamoja na mikoa mingine nchini ilikuwa na miti ya asili ya kila aina, hawawezi kuelewa kwa sababu hawana historia ya uoto wa asili kwa sehemu husika hivyo wanatakiwa kufundishwa kwa nadharia na vitendo ili waweze kwenda na wakati huu ambapo dunia nzima imekumbwa na mabadiriko ya tabianchi.

Anasema kwa kulitambua hilo, timu ya Uratibu wa Mradi wa Hifadhi Mazingira ya Ziwa (LVEMP 11) wakati wa kikao chake kilichofanyika jijini Mwanza, yeye pamoja na wataalamu kutoka LVEMP 11 alionelea kuchagua shule ya Sekondari ya Lumala iliyoko katika wilaya ya Ilemela jijini Mwanza,

Iweze kusaidiwa miche ya miti zaidi ya 280 ambayo zoezi la upandaji wa miti hiyo ufanywe na wajumbe wa Kamati ya LVEMP 11 kwa kushirikiana na uongozi wa shule hiyo, zoezi ambalo limefanikiwa kwa asilimia kubwa ili kurudisha uoto wa asili katika maeneo ya shule pamoja na wanafunzi kuweza kujifunza kwa vitendo juu ya utunzaji na uhifadhi mazingira kwa kupanda miti.

Naye Bw. Christopher Mafuru ambaye ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Lumala, anasema kuwa shule yake mbali na kutoa mafunzo mengine ya kawaida, imejikita zaidi katika shughuli za uhifadhi mazingira na kwamba tayari amekuwa akisimamia shughuli za upandaji miti lakini amekuwa akikabiliwa na changamoto kadhaa ambazo zimekuwa zikikwamisha shughuli za upandaji miti katika eneo la shule.

Anasema kuwa changamoto ambazo amekuwa akikumbana nayo ni pamoja na wananchi kuchungia mifugo katika eneo la shule na baadaye miche ya miti kuharibiwa na wanyama kwa vile shule yake haina uzio wa kuzuia wanyama kuingia katika eneo la shule.

Changamoto nyingine ni pamoja na baadhi ya miche kunyauka kutokana na mizizi yake kufikia katika miamba ambako ndio ukomo wa kuendelea kuota pamoja na shule yake kutokuwa na fedha za kuendeleza shughuli za upandaji miti ambazo zinafanywa na wanafunzi wapatao 80 kutoka shuleni hapo ambao wako katika kikundi cha Mali Hai.

Naye Bw John Masota ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ambayo inajishughulisha na upandaji miti kwa lengo la kutunza na kuhifadhi mazingira ya Environmental and Conservations ya jijini Mwanza, anasema kuwa taasisi yake imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika upandaji miti katika taasisi mbali mbali za serikali pamoja na watu binafsi.

Anabainisha kuwa katika kipindi kati ya mwaka 2009 hadi 2012, taasisi yake imepanda miti aina mbali mbali ipatayo 32,000 kwa kujitolea katika maeneo ya Jeshi la Wananchi Transit Cap Nyegezi mkoani Mwanza, miche mingine 15,000 imepandwa na taasisi hiyo katika maeneo ya Gereza Kuu Butimba, miche 15,000 imepandwa katika maeneo ya Hospitali ya Wilaya ya Butimba.

Anasema kwamba taasisi yake mpaka sasa inayo miche zaidi ya 5,000 ambayo inangojea kupandwa katika maeneo mbali katika mikoa ya kanda ya ziwa kutokana na mahitaji.

Anasema kwamba taasisi yake inakabiriwa na changamoto mbali mbali hususani kutokuwa na ushirikiano mzuri na baadhi ya watendaji wa serikali ambao mara nyingi wamekuwa wakikwamisha maendeleo ya upandaji miti hususani katika wilaya za Ilemela na Nyamagana.

Lakini katika kijiji cha Sakaya, Kata ya Lubugu, wilayani Magu, kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanziia Oktoba 2011 mradi wa upandaji miti aina ya Acasia Nilotica ambao umefadhiriwa na LVEMP 11, zaidi ya hekta 32 zimepandwa miche ya miti ipatayo 1,200. Mradi huo ni mmojawapo ya miradi ya kuhifadhi dakio la mto Simiyu ambao ulivumbuliwa na wanavijiji wilayani Magu.

Katibu wa Mradi, Bw Daudi Yakobo kutoka kata ya Lubugu anasema kuwa lengo la mradi huo ni kuongeza rutuba ya udongo na upatikanaji wa miti kwa ajili ya nishati, mbao, mkaa na chakula cha mifugo na wakati huo kupunguza uharibifu wa mazingira ambao unaendelea kukumba kata hiyo pamoja na vijiji vingine wilayani Magu pia kupunguza uchafuzi wa mazingira ya Ziwa Victoria kutokana na mto huo kutiririsha maji moja kwa moja katika ziwa hilo.

Anataja uharibifu uliokuwepo ambao ni pamoja na mmomonyoko wa udongo ambao huingia kwenye vyanzo vya maji kupitia vijito vya mto Mwamaganyala na Maganzuli na hatimaye kuingia mto Simiyu kupitia mto Duma na mradi huo umegharimu sh.20,572,979.00.

Juhudi za serikali kwa kushirikiana na wananchi za kuhifadhi na kutunza mazingira kama zitakuwa endelevu, zitasaidia kutokomeza uchafuzi wa mazingira na kurudisha uoto wa asili pamoja na kunusuru viumbe hai katika ziwa Victoria ikiwa ni pamoja na samaki na wanyama na viumbe wengine na kuongeza pato la Taifa na wananchi kujikwamua kiuchumi.


No comments:

Post a Comment