28 January 2013

Wasanii kupamba Siku ya Ma-Star kesho



Na Elizabeth Mayemba

WASANII wa Bongo flava nchini watashirikiana na wa Bongo muvi katika onesho maalumu la Usiku wa Ma-Star, linalotarajiwa kufanyika kesho katika Ukumbi wa Dar Live Mbagala, Dar es Salaam.

Onesho hilo limeandaliwa na Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) kwa kushirikiana na kampuni ya VANNEDRICK, ambapo watahudhiria wasanii mbalimbali wa muziki na filamu.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa TAFF Simon Mwakifwamba alisema onesho hilo ni maalumu kwa ajili ya kuchangia fedha kwa lengo la kujenga ofisi yao, pamoja na vitendea kazi muhimu vya ofisi.

Alisema wasanii mbalimbali wa Bongo flava, wamethibitisha kushiriki onesho hilo ambapo pia kuna baadhi ya wasanii wa filamu, watatoa singo zao kwa mara ya kwanza.

"Katika moja ya changamoto ya uendeshaji wa majukumu ya TAFF ni kukosa ofisi pamoja na vitendea kazi muhimu ndani ya ofisi, vifaa hivyo ni kama kompyuta, mikatati maalumu ya kuhifadhia nyaraka, mashine ya kudurufu, viti na meza za watendaji," alisema Mwakifwamba.

Alisema fedha inayotakiwa ni sh. milioni 60, hivyo kwa kupitia onesho hilo wana uhakika watafanikisha shughuli hiyo ya ukusanyaji wa fedha hizo, kwani ni muhimu katika shirikisho hilo.

Mwakifwambva alisema onesho hilo litaanza saa 6 mchana kwa burudani za watoto, ambazo zitadumu hadi saa 12 jioni na kiingilio chao kitakuwa ni sh. 2,000 na burudani kwa watu wazima zitafuatia ambapo VIP kiingilio kitakuwa sh. 15,000 na viti vya kawaida ni sh. 7,000.

Pia alisema burudani nyingi zitakazooneshwa ni zile zinazotokana na wasanii wenyewe wa filamu, ambao pia wanafanya na kazi za muziki, kupitia kundi la Shilole Classic, kundi la wachekeshaji likiongozwa na Mzee King Majuto, Kitale na Kingwendu.

Alisema Snura atakuwa na kundi lake, Hemed PHD, Masanja Mkandamizaji na  Alex wa Michejo, Afande Sele na bendi ya muziki wa dansi ya African Stars 'Twanga Pepeta'.

Wasanii wengine ni Jackline Wolper, Irene Uwoya, Aunt Ezekiel, JB, Rich Rich, Ray, Steve Nyerere na washereheshaji wa onesho hilo ni wadau wa filamu Ben Kinyaiya na Chiki Mchoma.

"Aidha tunatoa shukurani za dhati kwa kampuni zilizoanza kutoa ushirikiano hasa Kampuni ya Baucha Records, Global Publishers, ASET.co, Times FM, Steps Entertainment na VANNEDRICK Tanzania LTD.

No comments:

Post a Comment