15 January 2013

Wananchi wamshukia DC K'ndoni



Na Gladness Theonest

WAKAZI wa Mbezi Beach, eneo la Salasala, Dar es Salaam, wamemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Bw. Fotnatus Fwema, kutokutumia cheo chake kukandamiza wananchi wanyonge.


Wakizungumza katika mkutano uliofanyika mwishoni mwa wiki ambao uliitishwa na uongozi wa Serikali ya Mtaa wa Salasala, wakazi hao walimtuhumu Bw. Fweme kwa kumpa mwekezaji
eneo la barabara waliyokuwa wakiitumia muda mrefu.

Mkazi wa eneo hilo, Bw. Suleiman Malengai, alisema Bw. Fweme ameikuta barabara hiyo na kuhoji kwa nini aweke bango linalotoa siku 14 ambayo ndio mwisho wa kupita eneo hilo.

“Hii barabara ni ya asili na kisheria haipaswi kupewa mwekezaji kwani katika eneo husika kuna nguzo za umeme, viwanda, shule,
na makazi binafsi ya watu ambao hutegemea njia hii.

Wakazi hao walikosa imani na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Wazo, Bw. Raymond Chimbuya, ambaye alidai eneo la barabara hiyo linamilikiwa kihalali na mwekezaji ambaye alifidiwa na Wakala
wa Barabara nchini (TANROADS), ambao walipitisha barabara
katika eneo lake kwa kiwango cha lami.

“Mwekezaji amefuata taratibu zote za kisheria, nakala aliniletea ninazo hivyo amepewa eneo hili kihalali jambo hata jenga uzio eneo lote,” alisema Bw. Chimbuya mbele ya wananchi hao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Bi. Monica Timba, alidai kushtushwa na maandamamo makubwa
ya wananchi waliofika kwake kupeleka kilio chao ndio maana
akaamua kuitisha mkutano ili kujadili suala hilo.

Alisema Julai 2012, mwekezaji alitaka kuifunga barabara hiyo akidai manispaa hiyo ilimpimia upya hivyo ni mmiliki halali lakini baada ya kufuatilia, akabaini hakukuwa na ushirikishwaji kati ya Serikali Mtaa na wananchi wa Salasala.

Mwekezaji huyo, hakuweza kuhudhuria mkutano huo mbali ya kupewa taarifa hivyo wananchi walitoka na maazimio ambayo walikubaliana yatapelekwa manispaa ili yapatiwe majibu kabla
barabara hiyo haijafungwa.

Kutokana na tuhuma hizi, gazeti hili lilimtafuta Bw. Fweme ambaye alikiri kutoa kibali cha umiliki wa barabara hiyo kwa mwekezaji.

“Katika ramani ya mipango miji, barabara hii haipo kwa sababu imekatisha kwenye kiwanja cha mwekezaji na eneo ambalo linalalamikiwa si la wazi kama wanavyodai wananchi.

“Manispaa ndio yenye mamlaka ya kupanga matumizi ya ardhi
kwa kufuata michoro...mimi ndio mwenye dhamana ya kupanga matumizi ya ardhi kutokana na ramani...tatizo watu wamejenga mazoea ya kupita katika eneo hili na kuona la kwao,” alisema.

Alisema mwekezaji huyo ni mmiliki halali wa eneo ambalo linalalamikiwa na kama kutakuwa na mabadiliko yoyote katika barabara hiyo, Wizara husika ndiyo itakayotoa kibali.

No comments:

Post a Comment