16 January 2013

Wananchi Shy wampa ushauri JK


Na Suleiman Abeid, Shinyanga

KATIKA hali isiyo ya kawaida, mkazi wa Shinyanga, Bw. Deogratias Saimon, amemuomba Rais Jakaya Kikwete, aombe
ushauri kwa Rais wa Marekani, Bw. Barrack Obama, kuhusu
mbinu mbadala za kupambana na ugonjwa wa malaria nchini.


Alisema pamoja na Serikali kutoa vyandarua vya bure kwa
wananchi ili kupambana na ugonjwa huo mwaka 2011, hadi
sasa juhudi za mapambano hayo bado hazijafanikiwa.

Bw. Saimon aliyasema hayo hivi karibuni katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambao ulifanyika kwenye Viwanja vya Soko la Ngokolo Mitumbani, ili kutoa elimu ya uraia kwa wananchi.

Alisema katika uchunguzi wake, amebaini vyandarua hivyo vimeshindwa kupambana na ugonjwa huo nchini hivyo upo
umuhimu wa kutumia njia mbadala ili kuokoa maisha ya
Watanzania wengi ambao wanakufa kutokana na malaria.

“Vyandarua hivi kwanza havikuwa na ukubwa wa kutosha kulingana vitanda vinavyotumiwa na wananchi wengi pia vingi vimechakaa hivyo wananchi wanaendelea kuliwa na mbu kama ilivyokuwa
awali kabla msaada huo haujatolewa.

“Namuomba Rais Kikwete awasiliane na Rais wa Marekani (Obama), kama alivyofanya awali tukaweza kupata msaada wa vyandarua kwa ajili ya kuzuia ugonjwa huu lakini bado
havijatusaidia sana,” alisema Bw. Saimon.

Katika hatua nyingine, wananchi waliohudhuria mkutano huo waliwataka madiwani wa CHADEMA, kufikisha ujumbe wao
kwa uongozi wa Hospitali ya Mkoa ili waone umuhimu wa
kufanya usafi wa mazingira yanayozunguka hospitali hiyo.

“Tunaomba mtufikishie salamu hizi kwa uongozi wa Hospitali ya Mkoa wafanye usafi, vinginevyo wagonjwa wataendelea hapo
kuugua malaria kila siku, jambo hili linafumbiwa mamcho muda
mrefu, nyasi na nyingi hivyo kusababisha kichaka,” alisema.

No comments:

Post a Comment