21 January 2013

'Wana CCM jibuni mapigo ya wapinzani'


Na Severin Blasio, Morogoro

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Taifa (UWT), Bi. Sophia Simba, amewataka wana CCM  kufunguka na kujibu mapigo ya wapinzani ili kukijenga chama chao.


Aliwataka viongozi wa jumuiya hiyo, kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu 2015.

Bi. Simab ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo na Jamii, Jinsia na Watoto, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na viongozi wa UWT mkoani Morogoro.

“Hatuna budi kuyasema yote yanayofanywa na chama chetu ili kuwajulisha wanachama wetu na wapinzani ambao kila kukicha wanasema CCM haijafanya jambo lolote la maendeleo.

Alisema lazima Watanzania watambue kuwa, CCM imefanya mambo mengi ya maendeleo hususan ujenzi wa shule za sekondari za kata na barabara katika mikoa mbalimbali nchini.

“Wana CCM tumezidi ububu, hatujibu mapigo ya wapinzani ndio maana kila kukicha wanatusema...kwa nini tusiwajibu maneno yao, kuanzia sasa kila mwanachama bila woga awajibike kukisemea cham chaetu badala ya kukaa kimya,” alisema.

Bi. Simba aliitaka jumuiya hiyo kuacha kuwabagua wanawake kwa kigezo cha kutokuwa na kadi ya chama na kuongeza kuwa, UWT haikuundwa kwa ajili ya kikundi kidogo cha wanawake bali inawajumuisha wote wakiwemo wasio na chama ili kuwatetea.

“Tunapodai haki za wanawake hakuna ubaguzi wa kuangalia huyu na mwanachama au la...sisi ndiyo tumedai haki ya wanwake kupata elimu na kama mnalijua hilo, wanaopata elimusi wanachama wa UWT pekee bali ni wanawake wote,” alisema.

Aliongeza kuwa, kazi ya UWT ni kutetea haki za wanawake wote bila kujali itikadi ya vyama vyao kwani ukimwezesha mwanamke umeiwezesha jamii nzima.

Bi. Simba yupo mkoani humo kwa ziara ya siku katika Wilaya zote za Mkoa huo ili kutembelea wanachama na kuwashukuru kwa kuchaguliwa kwake katika nafasi hiyo.

No comments:

Post a Comment