21 January 2013

Hukumu ya Mchina mtoa rushwa yazua gumzo


Na Raphael Okello, Bunda

SAKATA la raia wa China aliyeshtakiwa kwa kutaka kumpa
rushwa ya sh. 500,000, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, mkoani Mara Bw. Joshua Mirumbe na kukwepa kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kulipa faini ya sh. 700,000, limeibua hisia tofauti
miongoni mwa wananchi juu vita dhidi ya rushwa nchini.


Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya wakazi wa Wilaya hiyo walidai kushangazwa na kesi hiyo kutolewa hukumu muda mfupi baada ya mtuhumiwa Bw. Mark Wang Wei, kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya, waakatio kesi nyingine za aina hiyo
hadi sasa hazijatolewa hukumu.

Mchina huyo alikamatwa Januari 16 mwaka huu, saa 7:30 mchana katika ofisi ya Bw. Mirumbe na Maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), ambapo kesho
yake alifikishwa mahakamani na kutolewa hukumu.

Baadhi ya wananchi, walipongeza uzalendo uliooneshwa na Bw. Mirumbe kwa kukataa kupokea rushwa na kuvishauri vyombo
vya dola kuharakisha kesi nyingine za aina hiyo.

“Kesi ya huyu Mchina, hukumu imetolewa ndani ya saa 24 tangu kukamatwa kwake hadi kufikishwa mahakamani, tofauti kesi nyingine kama hizi ambazo hadi sasa inadaiwa uchunguzi
unaendelea...hapa kuna nini,” alihoji Bw. Mwita Mabaga.

Alisema watuhumiwa wengi ambao kesi zao zinafanana na hizo, hadi leo hawajahukumiwa ambapo hali hiyo inakwamisha
mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Awali akizungumzia sakata hilo, Bw. Mirumbe aliwaambia waandishi wa habari kuwa, mapambano dhidi ya vitendo vya
rushwa yanahitaji uzalendo wa kila Mtanzania.

“Orodha ya kampuni zilizoletwa hapa wilayani na Wiazra ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa ajili ya zabuni ni kubwa lakini nilishangazwa na ujasiri wa huyu Mchina kuniletea rushwa.

“Binafsi naichukia rushwa, mtego niliomuwekea si kwamba yeye
ni raia wa nchi nyingine bali nilitaka vigogo waliopo nyuma yake watambue kuwa mimi sipendi rushwa ambayo ni adui wa haki,” alisema Bw. Mirumbe.

Aliongeza kuwa, mwaka 2012 kampuni zilizopewa zabuni ya kusambaza pembejeo hasa za mbegu ya pamba, ziliwadhurumu wakulima wilayani humo ambao walipata hasara kubwa wakati zenyewe zilipewa fedha nyingi na Serikali.

Bw. Mirumbe alizitaja kampuni ambazo tayari zimepewa zabuni ya kusambaza pembejeo wilayani humo ambazo ni SUBA-Agrotrading Co.Ltd, Tanseed, Tanzania Fertilizer Company na Minjingu.

Sakata la urasimu kwa mawakala wa pembejeo mwaka 2012, lilisababisha Bw. Mirunde atoe agizo la kusimamishwa kazi
watendaji wanane wa Serikali wilayani humo ambao kati yao, watano kutoka ngazi ya Wilaya akiwemo Ofisa Kilimo,
Uvuvi na Mifugo na watatu kutoka ngazi ya vijiji.

Bw. Wei ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Panda International Co. Ltd ya mkoani Shinyanga ambaye alitaka kumpa rushwa Bw. Mirumbe ili kampuni yake ipate zabuni ya kusambaza pembejeo.

1 comment:

  1. magamba wakati wa chaguzi mbalimbali Tanzania wanatoa hela 500000 kama hizo kwa mpiga kura mmojammoja ili wapigiwe kura nimeshudia mwenyewe kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani kata ya NANJARA REHA wilayani Rombo WAKISEMA WANATOA NI TAKRIMA NA SI RUSHWA KAMA NJIA YA KUTENGENEZA GOODWILL KWA WAPIGA KURA MCHINA NAYE ALITOA 500000 kwa mkuu wa wilaya MLIPWA FADHILA NA ALIYEMTEUA KUWA NI RUSHWA WAKATI MCHINA ALITOA TAKRIMA KUTENGENEZA GOODWILL KWAHIYO magamba haya yalimwonea MCHINA na pccb hilo ndilo waliliona?.

    ReplyDelete