21 January 2013

CHADEMA yawataka wanawake wasitishike



Na David John

MBUNGE wa Ubungo, Bw. John Mnyika, amelitaka Baraza la Wanawake la chama hicho (BAWACHA), kutoogopa vitisho ambavyo vinaenezwa na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwa mwaka huu utakuwa wa vurugu.


Hali hiyo inatokana na CHADEMA kuutangazia umma
kuwa, mwaka huu ni wa nguvu ya umma.

Bw. Mnyika aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akifungua Mkutano Mkuu wa BAWACHA uliofanyika Kata ya Saranga, Dar es Salaam na kuwataka wasitishwe na vitisho vinavyotolewa na viongozi wa CCM badala yake wapigane kuleta ukombozi wa Taifa.

Alisema propaganda zinazoenezwa na CCM zimelenga kuutisha umma hususan wanawake wasiunge mkono Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), kwani kujiunga kwao kwa wingi
kunadhihirisha jinsi wasivyo tayari kudanganywa.

Aliwaomba wanawake hao kwenda kutoa elimu kwa wengine kuhusu maana halisi ya falsafa ya chama hicho ya “Nguvu ya Umma”, ambayo imeelezwa katika katiba ya chama ibara ya 3.A kwamba wananchi ndio msingi na chimbuko la kuundwa kwa dola ya nchi ambapo umma ndiyo wenye madaraka ya mwanzo na mwisho ya kuamua hatima ya nchi na Taifa bila kuingiliwa wala kudanganywa.

Aliongeza kuwa, propaganda za CCM hivi sasa zimefikia ukomo wake hivyo mwaka 2013 ni wakati wa kutumia falsafa hiyo ili wananchi waweze kufanya maamuzi kuhusu rasilimali, uchumi
na siasa za nchi yao.

Bw. Mnyika alisema maandamano ni moja ya mbinu nyingi halali
za kidemokrasia katika kusimamia uwajibikaji kwa nguvu ya umma hivyo anaamini wanawake watajadili mbinu nyingine wakati wakisubiri ratiba ambayo itatolewa na chama hicho Taifa
kuhusu kazi za mwaka 2013.

“Nimeelezwa kwamba katika mkutano huu, mada mbalimbali zitatolewa, nitoe rai kwenu kuwa katika kuzijadili mada hizo na masuala yatayojitokeza mzingatie kauli mbiu ya BAWACHA kwamba wanawake ni chimbuko la maendeleo,” alisema.

Alisema mwaka huu ni kipindi cha kukamilisha uchaguzi wa
ndani, hivyo chama kitaendelea na maandalizi ya chaguzi
za vijiji, vitongoji na mitaa.

Alisema CHADEMA kinaamini kuwa, kumiliki rasilimali miongoni mwa wananchi kunawapa uhuru zaidi hivyo kwa itikadi hiyo ya mrengo wa kati, lengo ni kukijenga chama, Taifa lenye kutoa fursa na kuongoza nch.

No comments:

Post a Comment