03 January 2013
Walimu, wanafunzi wajisaidia vichakani
Na Eliasa Ally, Njombe
MBUNGE wa Ludewa, mkoani Njombe, Bw. Deo Filikunjombe (CCM), amesema kitendo cha Shule ya Msingi Lipangala, iliyopo wilayani humo kwa kukosa vyoo vya wanafunzi na walimu kwa
zaidi ya miaka mitano sasa, kinasikitisha na kuhuzunisha.
Hali hiyo inawafanya wanafunzi na walimu shuleni hapo kujisaidia vichakani hivyo upo uwezekano wa kupata magonjwa ya mlipuko.
Bw. Filikunjombe alionesha masikitiko hayo baada ya wananchi kumfikishia kilio hicho katika mkutano wa hadhara na kuuagiza uongozi wa Kata ya Lipangala, kukamilisha ujenzi wa vyoo vya wanafunzio na walimu ndani ya siku 10 kuanzia juzi.
“Nataka kuona shule hii ikifunguliwa, wanafunzi na walimu wakute vyoo vimejengwa na kuanza kuvitumia, kwa hali ilivyo sasa ni wazi kuwa utendaji kazi wa walimu unakuwa mgumu,” alisema.
Mkazi wa kata hiyo, Bi. Saraha Edward, alisema baadhi ya walimu hulazimika kurudi nyumbani kwao ili kwenda kujisaidia ambapo hali hiyo inawafanya muda mwingi kuwa nje ya ofisi hivyo kukwamisha maendeleo ya elimu shuleni hapo.
“Kama ujenzi wa vyoo katika shule hii utashindikana ni bora shule ifungwe, wazazi wana wasiwasi mkubwa juu ya afya za watoto wao kwani wanaweza kupata magonjwa ya mlipuko,” alisema.
Akizungumzia hali hiyo, Ofisa Elimu wa Tarafa ya Liganga,
Bw. Edward Wayotile, alithibitisha kuwepo kwa tatizo hilo na
kudai kuwa, tayari wameweka mkakati wa kujenga vyoo.
Aliitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kujenga vyoo vipya vyenye matundu 16 ambavyo vitatumiwa na wavulana, matundu
12 yatakayotumiwa na matundu mawili kwa matumizi ya walimu.
Kutokana na hali hiyo, Bw. Filikunjombe alikabidhi msaada wa
bati 50 kwa diwani wa kata hiyo ili kukamilisha ujenzi wa darasa
la awali na kumuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo
kutoa fedha za Mfuko wa Maafa kwa ajili ya ujenzi wa vyoo.
Mbunge huyo aliwataka wazizi wenye watoto waliofaulu kujiunga kidato cha kwanza 2013, kufanya maandalizi mapema na kutotumia fedha zote katika sherehe za kufunga mwaka.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment