03 January 2013

Adaiwa kujiondoa nyeti zake akitaka kujiua


Na John Gagarini, Kibaha

MKULIMA wa Visiga Kati, Wilaya ya Kihaba, mkoani Pwani,
Bw. Charles Malosha (44), amejiondoa nyeti zake akiwa katika
chumba cha mahabusu kwenye Kituo cha Polisi Visiga ambapo
tukio hilo limetokea Desemba 26 mwaka huu, majira ya mchana.


Akizungumza na gazeti hili jana katika Kituo cha Afya cha Mlandizi, Bw. Malosha mwenye watoto sita, alisema siku ya
tukio alichukuliwa na mgambo ambao walimwambia anahitajika kwenye Kituo cha Polisi Visiga.

Baada ya kufika kituoani hapo, aliambiwa kuna watu wanamdai fedha walizompa kwa ajili ya kuwauzia maeneo (ardhi).

“Wakati nikiwa kituoni, walifika walalamikaji wakiwa na polisi, mmoja kati yao alikuwa na rungu ambalo alinipiga nalo kichwani
nikapoteza fahamu na baada ya kuzinduka, nikakuta (Korodani), zangu zimekatwa na damu nyingi inamwagika hivyo
nikakimbizwa hospitali kwa matibabu,” alisema.

Bw. Malosha alikiri kudaiwa sh. milioni tatu na watu watatu
ambao walimpa fedha hizo ili awauzie maeneo lakini alishindwa kuwapatia baada ya wahusika kuyakataa kila alipowaonesha.

Mke wa Bw. Malosha ambaye alijitambulisha kwa jina la Bi. Martha Boni, alisema kuwa siku ya tukio, mumewe alimuaga nakudai hata muona tena hivyo alee watoto wake jambo ambalo lilimshangaza lakini hakuweza kumjua alikuwa na maana gani.

“Baada ya muda nilipigiwa simu na kuambiwa mume wangu yuko hoi hospitali na hawezi kuongea, nilichanganyikiwa na kutaka kujua yaliyomsibu lakini nilijulishwa kuwa ameondolewa sehemu zake za siri jambo ambalo lilizidi kuniumiza,” alisema.

Mganga wa Kituo cha Afya Mlandizi, Dkt,. Nicetus Matem, alisema alimpokea Bw. Malosha ambaye alifikishwa kituoni hapo akitokwa na damu nyingi na kujitahidi kuhakikisha inakata.

“Ni kweli korodanmi zake zimeondolewa kabisa na kitu kisicho na ncha kali na nilipomuuliza alisema amezinyofoa yeye mwenyewe,” alisema Dkt. Matem na kuongeza kuwa, mgonjwa huyo hawezi kuzaa tena ila atendelea kufanya tendo la ndoa kama kawaida.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Ulrich Matei, alisema taarifa walizonazo ni Bw. Malosha alijiondoa mwenyewe korodani zake
na alikuwa akidaiwa sh. milioni 11.5 na watu wanne tofauti.

“Aliachiwa shamba na bibi mmoja hivyo alikuwa akikata maeneo na kuyauza, mmiliki wa shamba alipofika alimwambia hakumpa ruhusa ya kuuza maeneo yake hivyo atajuana na watu waliompa fedha.

“Watu hao walianza kumdai kwa sababu aliwadanganya shamba
hilo ni la kwake hivyo walitaka kurejeshewa fedha zao, madeni yalimchanganya Bw. Malosha ambaye alitaja kujiua,” alisema.

Alisema lengo ni kutaka kujiua na hakufanyiwa kitendo hicho na mtu bali alijifanyia yeye mwenye.

No comments:

Post a Comment