04 January 2013

Wahasibu 4 Korogwe kortini kwa kutaka kuiba milioni 79/-


Na Yusuph Mussa, Korogwe

JESHI la Polisi Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, linawashikilia Wahasibu wanne wa halmashauri hiyo na mmiliki wa duka la vifaa vya ujenzi Bw. Mwalimu Jembe, kwa tuhuma za kutaka kuiba
fedha sh. milioni 79 kwa njia ya kughushi.

Akizungumza na mwandishi wa habari juzi kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Constantine Masawe, alikiri kukamatwa kwa watu hao lakini alikataa kuwataja majina akidai
jeshi hilo bado lipo katika uchunguzi wa kina.

Alisema watuhumiwa hao walitaka kuiba fedha hizo kwa hundi mbili tofauti, moja ya sh. milioni 41 na nyingine sh. milioni 37.9 mali ya halmashauri hayo.

Aliongeza kuwa, watuhumiwa walikamatwa usiku wa manane katika maeneo tofauti Desemba 31,2012 na bado wanaendelea kushikiliwa polisi.

“Tumewakamata Wahasibu wa vitengo mbalimbali kutokana na njama za kughushi sh. milioni 79, bado tupo kwenye mahojiano
nao, ushahidi ukikamilika tutawapeleka mahakamani,” alisema Kamanda Masawe.

No comments:

Post a Comment