04 January 2013

Ajali yaua watatu, 40 wajeruhiwa



Na Eliasa Ally, Mufindi

WATU watatu wamekufa papo hapo na wengine 40 kujeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya New Force Entreprises, kupata ajali katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya  Mufindi, mkoani Iringa.


Ajali hiyo imetokea jana saa nne asubuhi katika mlima mkali wakati likitokea mkoani Mbeya kwenda Dar es Salaam na lilipinduka mara mbili baada ya deresha wake kushindwa kulimudu kutokana na mwendo kasi.

Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Michael Kamuhanda, alisema waliokufa katika ajali hiyo ni wanaume wawili na mwanamke mmoja na miili yao
imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mufindi.

Aliwataka waliokufa kuwa ni Rogers Bonface (42), mkazi wa Mbeya, Anon Mwaijande (28), mfanyabiashara wa Mbeya na
Witnes Minja (25), mfanyabiashara wa Dar es Salaam.

“Dereva wa basi hili ni aina ya Yutong lenye namba za usajiri T 465 BBY, alishindwa kulimudu wakati akiteremka katika mlima ambao upo kwenye Kijiji Nyololo akielekeza Mjini Mafinga.

“Alipojaribu kufunga breki, lilitereza kwani barabara zimejaa maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mengi nchini,” alisema Kamanda Kamuhanda.

Alisema majeruhi wa ajali hiyo nao wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya Mufindi, wengine walitibiwa na kuruhusiwa kutokana na majeraha madogo waliyokuwa wameyapata.

Aliwataka madereva kuwa makini wanapoendesha vyombo
vya moto ili kuokoa maisha ya Watanzania wasio na hatia.

No comments:

Post a Comment