03 January 2013

Ukatili kwa watoto bado tatizo- utafiti



Na Rachel Balama

UKATILI dhidi ya watoto nchini limebainika kuwa ni tatizo kubwa ambapo wanawake 3 kati ya 10 na mwanaume 1 kati ya 7 wamewahi kufanyiwa ukatili kabla ya kufikia miaka 18.

Taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari na kusainiwa na ofisa kutoka Shirika la kimataifa la kuhudumia watoto la Save the Children Zanzibar Mubarak Maman kwenye matokeo ya utafiti yaliyoonesha kwamba Tanzania ni nchi ya kwanza katika Afrika kufanya utafiti wa kitaifa kuhusu ukatili wa watoto.

Ilisema kuwa utafiti huo kwa mara ya kwanza uliweza kupima aina zote za ukatili ukiwamo wa ngono, kimwili na kiakili wanaofanyiwa wavulana na wasichana na kutoa makadilio ya kitaifa ya kiwango cha ukatili.

"Katika utafiti huo ilibainika kuwa karibu robo tatu ya wanaume na wanawake wamewahi kufanyiwa ukatili kabla ya umri wa miaka 18 na watu wazima au na jamaa zao wa karibu na robo moja wamesababishiwa na mtu mzima ukatili wa kifkira," ilisema taarifa.

Aidha ilisema kuwa ingawa kiwango cha ukatili Zanzibar kipo chini ambapo karibu asilimia 6 ya wanawake na asilimia tisa ya wavulana wamefanyiwa ukatili.

Taarifa hiyo ilisema ukatili wa kingono dhidi ya watoto ni swala linalohitaji kushughulikiwa mapema na kwamba matokeo ya utafiti huo yana maana za msingi kwa Tanzania katika upangaji na utekelezaji wa mipango maalumu ya kuzuia na kukabiliana na ukatili na kuwatumia matumizi mabaya dhidi ya watoto. 

"Utafiti uliofanyika Zanzibar (ZVCS) ulionyesha kwamba kuna tatizo kubwa kutokana na takwimu na taarifa zilizokusanywa juu ya kiwango cha ukatili na uzito wake hapa visiwiani, matokeo yalionyesha kwamba watoto wa umri wote wamo katika hatari ya kunyanyaswa na kunyonywa kiuchumi," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Ilisema kuwa ukatili dhidi ya watoto kutumiwa kingono na unyanyasaji ni matatizo ya msingi na yanatokea katika mazingira mbalimbali hapa Zanzibar iwe nyumbani, shuleni na ndani ya jamii.

Aidha ilisema kuwa ili kufanikisha hili, kunahitajika nguvu za pamoja za Serilali, mashirika yasiyo ya kiserikali na vyombo vya habari.

"Kampeni ya kuzuia na kukabiliana na ukatili dhidi ya watoto inatambua umuhimu wa kutoa ulinzi bora kwa watoto wa Zanzibar dhidi ya ukatili nyumbani, shuleni na katika jamii ukatili ambao siku zote hufanyika bila kuonekana," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Hata hivyo ilisema jitihada za pamoja zitahakikisha kuwa watoto wanaweza kupata huduma nyingine za kimaisha kama vile afya, malezi, na usafi pamoja a huduma za ulinzi ambazo zinabainisha na kuwalinda watoto dhidi ya vitisho na madhara wanayoweza kupata kutokana na ukatili na unyanyaswaji.

No comments:

Post a Comment