28 January 2013

Vijiji vitatu vyadaiwa kutaka kuanzisha vurugu tena Kilosa


Severin Blasio, Kilosa

BAADA ya kuzuka vurugu katika eneo la Dumila wilayani Kilosa hali si shwari katika vijiji vya Kilangali,Kivungu na Mbamba kata ya Kilangali wilayani humo baada ya shamba la Summer Grow walilokuwa wakilima wananchi wa vijiji hivyo kupewa
wafugaji.


Akizungumza na waandishi wa habari mchungaji wa kanisa la Anglikana  Anold Mwegoha alisema kuwa shamba hilo lenye ukubwa wa zaidi ya heka 2500 lililokuwa la mkonge na lilitelekezwa na kampuni hiyo miaka saba iliyopita na wakulima wa vijiji hivyo kuanza kulima, lakini kudai kuwa uongozi wa wilaya ya Kilosa umewapatia wafugaji jambo ambalo linaweza kusababisha vurugu baina ya pande hizo mbili.

Mchungaji Mwegoha alisema kuwa hali kwa sasa si shwari kutokana na wakulima kung'ang'ania eneo hilo huku wafugaji nao wakiendelea na shughuli za ufugaji bila kujali kuwepo kwa mazao kwenye mashamba hayo.

"Hivi karibuni mkuu wa wilaya ya Kilosa alifika eneo hilo na kuzungumza na wananchi na kuagiza wakulima kuacha kuendelea kulima na kwamba eneo hilo wamepatiwa wafugaji hatua ambayo imepingwa na wakulima na kusema kuwa watendelea na kilimo hata kama wamezuiwa kufanya hivyo"alisema.

Aliongeza kuwa kwa sasa wananchi wa kijiji cha Mbamba inadaiwa kuwa wameanza kujifua kwa kutumia walinzi wa jadi maarufu kama Uwajaki kwa lengo la kujiandaa kwa lolote ambalo linaweza kujitokeza baina yao na wafugaji jambo ambalo linapaswa kuangaliwa haraka na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na serikali ya wilaya na mkoa.

Hata hivyo kiongozi huyo wa kanisa alisema viongozi wa dini wamekuwa wakifanya jitihada za kuwasihi wananchi kuacha kufanya vurugu badala yake waendelee na jitihada za kuwaona viongozi wa serikali ili kutatua kero hiyo.

Wakati huo huo vurugu zilizojitokeza juzi Dumila  katika vijiji vya Mfuru,Masanze na Vikenge wilayani Mvomero kutaka kupewa ardhi ya kitongoji cha
Mabwegere ambayo inadaiwa kupewa wafugaji huku wakidai kuwa wakulima walishinda na
kupewa eneo hilo imekwisha.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa  kamanda wa polisi mkoani Morogoro Faustine Shilogile alisema, kuwa hali kwa sasa ni shwari na kwamba hakuna mauaji wala majeruhi.

"Pamoja na kwamba wananchi walikuwa na wasiwasi kuhusiana na vurugu hizo kuwa huenda wafugaji wakalipiza kisasi kutokana na nyumba na biashara za wafugaji kuharibiwalakini hakujajitokeza vurugu zozote kutokana na askari polisi Kikosi cha Kuzuia
Ghasia(FFU) kuimarisha ulinzi katika maeneo yote.

Katika vurugu za jana kwenye kijiji cha Dumila Mtu Mmoja Mohamed Msigala(60) alipoteza maisha kutokana na mstuko alioupata ulisababishwa na mabomu 

Vurugu hizo zilisabababisha nyumba kadhaa za wafugaji kuharibiwa pamoja na biashara zao na watu kadhaa kujeruhiwa baada ya wananchi hao kufunga barabara ya Morogoro Dodoma kwa masaa zaidi ya matatu.

Wananchi hao walikuwa wakishinikiza uongozi wa mkoa kwenda kusikiliza kero yao ya kupolwa ardhi ya kijiji cha Mabwegere na kupewa wafugaji na baadaye uongozi wa wilaya hiyo ukiongozwa na mkuu wa wilaya ya Kilosa Elias Tarimo kufanya mkutano na wananchi jumapili ya wiki iliyopita na kutamka kuwa eneo hilo ni la
wafugaji kisheria.




No comments:

Post a Comment