28 January 2013

Serikali yashauriwa kuacha kuwakumbatia wawekezaji



Na Suleiman Abeid,
Maswa

MWANAFUNZI anayesoma kidato cha tatu katika shule ya sekondari Mataba wilayani Maswa mkoani Simiyu Christopher Andrea ameishauri serikali iache mtindo wa kuwakumbatia wawekezaji wa kigeni vinginevyo Tanzania itageuka kuwa nchi ya kibebari.


Andrea aliyekuwa akitoa maoni yake juzi katika Mdahalo wa utoaji maoni juu ya katiba
mpya kwa makundi maalumu ulioandaliwa na Muungano wa Azaki za kiraia wilayani Maswa (MASWANGONET) mjini Malampaka alisema Tanzania isipobadili mfumo wa kuwapendelea wawekezaji ipo hatari ya kurejea katika enzi za ubepari.

Alisema baada ya Tanzania kuruhusu mfumo wa uwekezaji serikali imekuwa ikitoa upendeleo mkubwa kwa wawekezaji wa nje huku ikiwapuuza wazawa na mara nyingi hutumia nguvu kubwa kuwafukuza katika ardhi wanazomiliki wakitakiwa kuwapisha wawekezaji na wawekezaji hao wakipewa misamaha ya kodi.

Alisema daima wawekezaji wanaokuja kuwekeza hapa nchini hawana mapenzi na watanzania bali wanachojali zaidi ni kuchuma faida kutoka katika raslimali zilizopo nchini na kuzipeleka katika nchi zao ambako hukuza uchumi wa nchi hizo na watanzania wengi wakibaki kuwa watazamaji.

“Mimi kwa upande wangu napendekeza katiba ijayo iweke ibara itakayowalinda wazawa wasinyanyashwe na wawekezaji katika nchi yao, na pia serikali iache kutoa upendeleo mkubwa kwa wawekezaji maana tusipokuwa makini nchi yetu itakuwa ni ya kibepari wengi tutageuka manamba wa kuwatumikia wao,” alisema Andrea.

Kwa upande wa suala la elimu mwanafunzi huyo alipendekeza serikali ichague lugha rasmi ya kufundishia mashuleni kuanzia madarasa ya chekechea hadi chuo kikuu ambapo alisema hivi sasa watoto hushindwa kufanya vizuri katika mitihani yao kutokana na kuchanganya lugha.

“Mimi naona hili suala la lugha ya kufundishia ni vizuri likatajwa rasmi ndani ya katiba ijayo, maana hivi sasa kuanzia madarasa ya chekechea watoto wanafundishwa kwa lugha ya kiswahili, lakini wakianza sekondari wanafundishwa kwa kiingereza, hili ni tatizo, kumuanzishia mtoto lugha mpya inamchukua muda kuielewa,”

“Sasa ni vizuri kama ni kiswahili basi kianzie madarasa ya chekechea hadi chuo kikuu, na kama ni kiingereza basi iwe kitumike kufundishia kuanzia madarasa ya chekechea, kuchanganya lugha za kufundishia ni tatizo linalochangia matokeo mabaya
mashuleni kila mwaka,” alisema Andrea.

Aidha washiriki wa mdahalo huo uliofadhiliwa na Shirika la The Foundation For Civil Society walipendekeza katiba mpya ijayo iweke ukomo wa eneo la ardhi itakayokuwa ikitolewa kwa wawekezaji kutoka nje na kwamba kiwango cha mwisho kiwe ni ekari 100.



No comments:

Post a Comment