28 January 2013

Vibonde wa Yanga waitafuna Simba


Na Elizabeth Mayemba

MABINGWA wa Tanzania Bara Simba jana walifungwa bao 1-0 na timu ya Afrika Kusini katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Timu hiyo ya Leopards, ambayo inacheza Ligi Kuu nchini Afrika Kusini, imefungwa mara mbili na Yanga ambapo katika mechi ya kwanza iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ilifungwa mabao 3-2 na mechi nyingine iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ilizabwa mabao 2-1.

Leopards ndiyo ilianza kupata bao dakika ya saba baada ya beki wa Simba, Hashim Isihaka kujifunga wakati akijaribu kuokoa hatari iliyopigwa langono mwake kwa mpira wa krosi iliyochongwa na Kodney Ramagalela.

Hata hivyo katika mechi hiyo Simba ilicheza timu ya vijana, ambapo wachezaji waliokuwepo na timu nchini Oman waliocheza katika mechi hiyo ni Ramadhan Singano 'Mesi', Hassan Khatibu na Rashid Ismail.

Simba walikosa bao dakika ya 17, baada ya Singano kupiga shuti kali lililogonga mtaa wa panya na mpira kutoka nje.

Dakika ya 45 Simba ilikosa bao la wazi baada ya Rashid Ismail, akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga kupiga shuti nje ya 18 lililotoka nje ya lango.

Kipindi cha pili, Simba ilicharuka kwa kuliandama lango la wapinzani wao lakini, wachezaji wake hawakuwa makini katika umaliziaji.

Kocha wa Simba Patrick Liewing, aliamua kuwachezesha wachezaji wa timu B, ili kuwapumzisha wachezaji wa kikosi cha kwanza kwa ajili ya kuwapa nafasi ya kujiandaa vyema na mechi ya Ligi Kuu mzunguko wa pili inayotarajiwa kuanza kesho.

Simba ilirejea nchini juzi ikitokea nchi, Oman ambako iliweka kambi ya wiku mbili kwa ajili ya kujiandaa na Ligi Kuu.

No comments:

Post a Comment