28 January 2013

TBL yamwaga vifaa Simba, Yanga


Na Elizabeth Mayemba

KLABU za Simba na Yanga, jana zimekabidhiwa vifaa vya michezo vyenye thamani ya sh. milioni 70 na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Kilimanjaro kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, unaotarajiwa kuanza kesho.


Akikabidhi vifaa hivyo Meneja wa bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema vifaa hivyo ni sehemu ya udhamini wao kwa klabu hizo kubwa nchini, ambapo kila moja ilipata vifaa vyenye thamani ya sh. milioni 35.

"Bila shaka Simba na Yanga, ndiyo klabu kubwa zaidi hapa Tanzania zikiwa kwa pamoja, zimeweza kupata mafanikio makubwa kwa kipindi kirefu na bado zinaendelea kufanya vizuri, tunajivunia kuweza kuziunga mkono klabu hizi katika jitihada za kuwania taji la Ligi Kuu msimu huu," alisema Kavishe.

Vifaa vilivyotolewa jana ni mipira, viatu, soksi, vizuia ugoko, nguo za mazoezi na vitu vingine ambavyo vitaziwezesha timu hizo kucheza wakifurahia kuvaa vifaa vyenye ubora wa hali ya juu.

Aliongeza kuwa udhamini wao kwa klabu hizo kongwe nchini, umesimamia katika misingi ya kufanya kazi pamoja, uadilifu na kuendelea kupata mafanikio.

Akipokea vifaa hivyo Msemaji wa Klabu ya Simba, Ezekiel Kamwaga aliwashukuru wadhamini hao ambapo alidai vifaa vya safari hii, hasa mipira ni ile ambayo inatumika kwa sasa duniani kote, hivyo wachezaji wao watafurahia zaidi.

"Tunawashukuru TBL kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro na sisi tunawaahidi kufanya vizuri zaidi, katika Ligi Kuu na michuano ya kimataifa na mwaka huu kwetu sisi, Simba ni wa mafanikio kwani miaka yote inayoishia tatu mwishoni huwa tunakuwa na mafanikio makubwa sana," alisema Kamwaga.

Naye Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alitoa pongezi zake kwa wadhamini hao na kuahidi kushirikiana nao, ikiwa na kuleta changamoto kubwa katika ligi ili kutowakatisha tamaa wadhamini wao.

"Sisi kama Yanga, tunajivunia kuwa na mdhamini anayejali hivyo na sisi tunatakiwa tusiwaangushe, pia tunaahidi mwaka huu kuchukua ubingwa wa ligi, ili mwakani tushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika," alisema Mwalusako.

No comments:

Post a Comment