28 January 2013

Ushirikiano kwa Jeshi la Polisi unaimarisha usalama nchini-Mwema



Na Stella Aron

MATUKIO ya uhalifu nchini yameonyesha kupungua kutokana na ushirikiano mzuri kati Jeshi la Polisi na wananchi kwa kutoa taarifa za uhalifu.


Kwa ujumla hali ya uhalifu nchini imeendelea kudhibitiwa katika makosa makubwa ya jinai licha ya ongezeko dogo la idadi ya makosa ya usalama barabarani.

Jeshi la Polisi nchini Tanzania limepewa majukumu ya kulinda amani, kusimamia utekelezaji wa sheria na kanuni za nchi,
kuzuia na kuepusha makosa kabla hayajatendeka kukamata wahalifu na kuwafikisha mahakamani na kulinda mali za raia na za umma.

Inspekta wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema anasema kuwa majukumu hayo ndiyo msingi mkuu wa kudumisha sheria,haki na amani.

Kamanda Mwema anasema kuwa awali Jeshi la Polisi lilidumu kwa kiasi kikubwa kupambana na uhalifu lakini kutokana na kukuwa kwa sayansi na teknolojia,miingiliano ya watu na shughuli za binadamu, kuporomoka kwa maadili ndani ya jamii na jukumu la kupambana na uhalifu kwa kulitegemea Jeshi la Polisi peke
yake linaonekana wazi kuwa ni gumu.

Kutokana na changamoto hiyo Kamanda Mwema anasema kuwa ili kudumu mapambano hayo ya uhalifu liliamua kufanya mabadiliko na maboresho makubwa ya kiutendaji ndani na nje ya Jeshi.

Kamanda Mwema anasema kuwa katika mhimili wa
polisi jamii na ulinzi shirikishi ndiyo una lengo kuu la kushirikisha jamii katika kujilinda. Aidha, programu hii inasisitiza suala la ulinzi ili kuimarisha usalama wa maeneo yao ya kihusisha makazi, sehemu za kazi, biashara na maeneo yoyote yale ambayo ni muhimu kwa Taifa.

Anasema kuwa katika kuhakikisha kuwa uhalifu unapungua hapa nchini jeshi hilo limejikita zaidi katika suala la ulinzi shirikishi ili kujenga mahusiano mazuri kati ya polisi kwa
kushirikiana pamoja na raia, asasi mbalimbali ili kupambana na kutatua matatizo ya uhalifu.

Anasema kuwa falsafa ya Polisi Jamii na ulinzi shirikishi ndani na nje ya Jeshi la Polisi kwa kiasi kikubwa imechangia kukuza uhusiano na wananchi na hivyo kuwafanya wawe huru kutoa taarifa za uhalifu bila woga.

Kwa kuwepo kwa kitendo hicho jeshi hilo limefanikiwa kubaini maeneo ya uhalifu, kuwatambua wahalifu na kugundua vyanzo vya makosa.

Pamoja na kuwepo kwa mafanikio hayo Kamanda Mwema anasema kuwa bado jeshi hilo linakabiliwa na tatizo la vitendea kazi, upungufu wa askari katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

Anasema kuwa uwiano kati ya askari na idadi ya watu anaowahudumia pamoja na ukubwa wa maeneo mraba ni mkubwa kwa askari kutoa huduma ipasavyo hivyo kutokana na tatizo hilo wastani wa askari mmoja uhudumia watu 1,294 ni mkubwa, huku maeneo yakitofautiana kijiografia kulingana na mikoa.

Anasema kuwa uhaba wa askari Polisi na vitendea kazi unaosababishwa na ukubwa wa
maeneo ya mikoa husika ambapo ukweli huo unadhihirika kutokana na kesi zilizoripotiwa na kushughulikiwa ambapo kesi nyingi zipo chini ya upelelezi ikilinganishwa na kesi
zilizofikishwa mahakamani.

Aidha bado jitihada zinahitajika katika kuhakikisha kasi ya usukumaji kesi
inapewa kipaumbele na takwimu zinaonyesha kuwa kesi za nyuma bado ni mzigo kwa upande wa mahakamani na polisi ambazo zipo chini ya upelelezi.

Kamanda Mwema anasema kuwa kutokana na suala hilo ni bora waajiriwe askari wakutosha kulingana na ujenzi wa vituo vya Polisi vinavyoendelea kujengwa sehemu mbalimbali ya nchi ili kwenda sambamba na ongezeko la idadi ya watu, siyo tu ajira bali pia mafunzo kwa
wapelelezi na idadi yao iongezwe kulingana na
ukubwa wa kesi katika mikoa husika.

Kamanda Mwema anasema kuongezewa vitendea kazi hususani magari pamoja na bajeti kutasaidia kukidhi mahitaji ambayo yatawezesha utendaji makini na

Anasema kuwa huduma bora za ulinzi na usalama wa kutosha wa wananachi wake na mali zao ili huduma zote muhimu ziweze kutekelezwa kwa amani na utulivu.

Katika kuhakikisha kuwa wananchi wanaishi kwa amani na usalama Jeshi la Polisi limeweza kujipanga na kukabiliana na uhalifu wa aina zote licha ya uhaba wa rasilimali.

Naye Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Isaya  Mnguru anasema kuwa kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Novemba, mwaka jana ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2011 takwimu zinaonesha hali ya uhalifu imepungua.

DCP Mnguru anasema kuwa hali ya mwenendo wa uhalifu kwa mwaka jana makosa makubwa ya jinai yaliyotolewa taarifa katika vituo vya polisi ni 66,255 ikilinganishwa na makosa 69,678 yaliyo ripotiwa kwa kipindi cha mwaka 2011 ni upungufu wa makosa 3,423 ambao ni sawa na asilimia 4.9.

Mnguru anasema kuwa matishio ya usalama nayo yamepungua kwani mpaka sasa hakuna tishio la dhahiri hapa nchini kuhusiana na tishio la ugaidi.

Alisema hali hiyo imetokana na hatua zilizochukuliwa katika kuimarisha ulinzi kwenye mipaka na maeneo nyeti sambamba na kuwatahadharisha wananchi kuwa waangalifu na kutoa taarifa za nyendo za watu au vikundi wanavyovitilia mashaka.

Anaongeza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kubuni na kutekeleza kikamilifu mikakati ya kukabiliana na uhalifu ikiwemo kushirikiana na wadau wote wa ulinzi na usalama katika kubadilishana taarifa za kiintelijensia pamoja na uzoefu wa kuzuia uhalifu kwa kuibua mifumo mipya na kuboresha ya zamani.

Anasema kuwa katika kuhakikisha kuwa uhalifu unapungua namba za simu za makamanda wa polisi zimesambazwa nchini kote wananchi wasisite kuzitumia wapoona viashiria vya uhalifu.

Hata hivyo Kamanda Mwema aliwaonya wale wote wasiopenda kutii sheria kwa hiari yao kuacha tabia hiyo wakiemo madereva wa mabasi ya abiria kutotii sheria za barabarani pamoja na waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda kutovaa kofia ngumu na kupakia abiria zaidi ya mmoja.

Katika kuhakikisha kuwa uhalifu unapungua nchini Kamanda Mwema alimkabidhi pikipiki Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kama ishara ya kukabidhiwa makamanda wote Tanzania bara na Visiwani.

IGP Mwema anasema jumla ya Pikipiki 564 zimekabidhiwa kwa ajili ya kuzuia uhalifu kwa lengo la matumizi ya Wakaguzi Tarafa wa Polisi Tanzania bara na Majimbo yote ya Zanzibar, program za Safiri Salama na Usalama wetu kwanza.

Anasema kuwa vifaa hivyo vya usafiri ni moja ya hatua za wizara hiyo kupunguza matukio ya uhalifu nchini na kutoa elimu kwa wananchi juu ya ulinzi shirikishi.

Inspekta Mwema anasema kuwa pikipiki hizo zitatumika kuzuia uhalifu katika jamii na kwamba wananchi wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa Polisi ili kusaidia ulinzi na usalama wa raia.

Anasema pikipiki hizo zitasaidia katika kuzuia uhalifui kabla ya kutokea, baada ya uhalifu kutokea na kupelekwa kwa mhalifu polis, mahakamani na hamimaye gerezani,

Anasema kuwa huo ni mpango wa kupunguza na kuzuia uhalifu kuanzia ngazi ya familia moja mpaka ngazi ya wilaya na watahakikisha kwa kiasi kikubwa zinatumiwa kwa madhumumuni husika na kupamba na uhalifui.

Anasema pikipiki 29 zimetolewa kwa askari wa doria barabarani, 9 kwa Kikosi cha Usalama ambacho kinatoa elimu mashuleni na 526 kwa wakaguzi wa tarafa nchi nzima Tanzania bara na visiwani.

2 comments:

  1. JESHI LA POLISI LIJIPANGE UPYA UCHOMAJI WA NYUMBA KIBITI ,DUMILA NA MTWARA JAMII IMEJAA CHUKI ZA UBAGUZI WA KIDINI NA KIKANDA TUSIITENGENEZE SOMALIA HAPA

    ReplyDelete
  2. polisi jamii mafia kisiwani imeeleweka na kukubalika kwani baadhi ya wananchi wameipokea vizuri,,hivi sasa kuna vikundi vya ulinzi shirikishi

    ReplyDelete