03 January 2013
Pinda apewa tuzo ya Mkoa wa Katavi *Atangazwa rasmi kuwa Mfalme wa Nyuki
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amepewa Tuzo ya Heshima ya Mwaka 2012 ya Mkoa wa Katavi katika vipengele viwili vya Utawala Bora na Uhamasishaji wa ufugaji nyuki.
Waziri Mkuu alipokea tuzo hizo usiku wa kuamka juzi kwenye hafla ya kuuaga mwaka 2012 na kuukaribisha mwaka 2013 iliyofanyika kwenye ukumbi wa Idara ya Maji mjini Mpanda, mkoani Katavi. Alikabidhiwa cheti cha tuzo hiyo na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dkt. Rajab Rutengwe.
Akitoa maelezo ya utangulizi kabla ya kutangaza majina ya watunukiwa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi,Mhandisi Emmanuel Kalobelo alisema mkoa wa Katavi umeamua kuanzisha mfumo wa utoaji wa Tuzo ya Mkoa kwa lengo la kuwatambua,kuwatia moyo na kuwapa motisha wananchi na watumishi wa umma waliofanya vizuri katika nyanja mbalimbali za utoaji wa huduma kwa wananchi.
"Tuzo hii itaendelea kutolewa kila mwisho wa mwaka...Tumeamua kufanya hivi ili kuamsha ari kwa wengine kufanya vizuri zaidi mwaka unaofuata," alisema.
Sekta zilizopewa tuzo ni mapato na kodi za Serikali, utawala bora, uchumi na maendeleo, Ulinzi na usalama, mipango miji, mawasiliano na teknolojia, ufugaji nyuki na hifadhi ya mazingira, elimu, kilimo na mifugo, michezo, usafirishaji
na huduma za jamii.
"Waziri Mkuu Mizengo Pinda anatunukiwa tuzo ya utawala bora,siasa safi na ushiriki katika
shughuli za maendeleo ya wananchi wa jimbo lake la Katavi na Ukanda wa Ziwa Tanganyika kikamilifu,"
"Tuzo ya pili ni ya kumtambua kuwa mfugaji nyuki na mhamasishaji kichocheo wa kitaifa wa ufugaji nyuki. Sisi wana-Katavi tunakutambua kama Mfalme wa Nyuki nchini," aliongeza.
Wengine waliopewa tuzo katika hafla hiyo ni Bw.Deus Assenga, Bw. Michael M. Tarimo wa M.M (2001) Group Ltd na Bw. Shabir Hassanali Walimohamed ambao walitambuliwa kama Walipakodi Bora Mkoa wa Katavi mwaka 2012 kwenye kipengele cha Mapato na Kodi za Serikali.
Wengine ni Bw. Paschal Kweya aliyepewa tuzo katika ubunifu wa usafi na hifadhi ya mazingira Mkoa wa Katavi ambaye aliiwezesha Halmashauri ya Mji kuwa mshindi mara mbili mfululizo 2011 na 2012.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment