21 January 2013

TWB kufungua tawi la pili KariakooNa Amina Athumani

BENKI ya wanawake nchini (TWB) inatarajia kufungua tawi lake la pili maeneo ya Kariakoo mwezi Februari mwaka huu baada ya kufikisha mtaji wa sh. bilioni 6.8 tangu kuanzishwa kwa benki hiyo miaka mitatu iliyopita.

Akizungumza Dar es Salaam jana, makao makuu ya benki hiyo kuhusiana na benki hiyo kupanua shughuli zake, Mkurugenzi Mtendaji wa TWB, Bi.Magreth Chacha alisema benki hiyo sasa inaanza kupanua wigo wake kwa kujenga matawi nchini.

Bi.Chacha alisema kuwa kwa kuanzia wanafungua tawi la benki ya wanawake maeneo ya kariakoo ili kuwapa urahisi wateja wao kuchukua fedha na kufanya manunuzi kwa urahisi.

"Kwa kipindi kifupi benki imeweza kufanya vizuri kiasi cha kupata kibali cha kufungua tawi la pili Kariakoo na kuanzisha vituo vya mikopo katika mikoa miwili ya ya Mwanza na Dodoma na tunategemea kufanya uzinduzi rasmi wa vituo hivyo mwishoni mwa mwezi huu,"alisema.

Alisema tawi la mjasiriamali Kariakoo kama lilivyo la kwanza la Mkwepu litatoa huduma zote za kibenki ikiwemo kupokea Amana na kutoa mikopo.

"Wananchi wote wanakaribishwa hasa wajasiriamali wanaojishughulisha na biashara ndani ya kariakoo ambao mwanzo walishindwa kuweka akiba zao kwa sababu ya umbali wa tawi letu,"alisema.

Alisema benki hiyo hutoa huduma za kibenki ikiwa pamoja na kutuma hela nje ya nchi kwa mtandao wa SWIFT, TISS, Western Union na M-Pesa.

Alisema benki hiyo imeweza kutatua changamoto zinazowakabili wajasiriamali wadogowadogo kwa kuwapatia mikopo yenye riba nafuu, masharti nafuu katika vikundi na marejesho nafuu katika kipindi cha wiki hadi mwaka.

Alisema mpaka sasa wateja wa TWB, wanaendelea kufaidi hifadhi zao kwa kupitia ATM zaidi ya 150 zilizopo nchi nzima kupitia mtandao wa umoja Swich ambayo TWB ni mwanahisa wa benki hiyo.

Alisema tangu kufunguliwa kwa benki ya TWB, mpaka Desemba mwaka jana imeweza kuwa na wateja 30,000 wanawake wakiwa ni asulimia 77 na wanaume asilimia 23 wenye amana zenye thamani ya sh. Bilioni 16.2 na imeweza kuwanufaisha wateja zaidi ya 25,000 kwa njia ya mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 33 na hiyo imetokana na kukua kwa biashara na kuboresha maisha ya wajasiriamali.

Alisema pia wajasiriamali katika vikundi wamenufaika na mafunzo ya uwendeshaji biashara na mikopo nafuu kwa kiasi cha sh. bilioni 14 tangu kuanza kwa shughuli za mikopo.

Wazo la kuanzishwa kwa benki hiyo ya wanawake lilikuwepo tangu mwaka 1999  na mwaka 2009 ilianzishwa rasmi na kusajiliwa ikiwa na hisa ya sh. bilioni 2.8 zilizotolewa na Serikali chini ya Rais Jakaya Kikwete ambaye aliahidi kutoa kiasi cha sh. bilioni 2 kila mwaka wa fedha kwa kipindi cha miaka mitano cha awamu yake.

No comments:

Post a Comment