21 January 2013

Tusiwahukumu wananchi wa Mtwara
Na Danny Matiko

ITAKUMBUKWA kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania wananchi waliandamana mkoani Mtwara Desemba 27, mwaka jana, kupinga gesi-asili inayochimbwa mkoani humo kusafirishwa kwa njia ya bomba mpaka Dar es Salaam.


Kadhalika, itakumbukwa kuwa kabla ya kufanyika maandamano hayo, uzinduzi wa mradi huo wa serikali ulifanywa na Rais Jakaya Kikwete Novemba 8 mwaka jana Dar es Salaam, hiyo ikiwa ni ishara ya kukamilika mipango ya kuanza kazi ya ujenzi wa mabomba yatakayosafirisha gesi hiyo.

Bomba lenye kipenyo cha sentimeta 91 (inchi 36) na urefu wa kilometa 532 kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam litapita katika mikoa ya Mtwara yenyewe, Lindi, Pwani na Dar es Salaam.

Mradi huo pia umevuta hisia za kimataifa, ambapo hata gazeti maarufu la "Independent" la nchini Ireland liliripoti hivi karibuni kuwa, "kugunduliwa kiasi kingi cha gesi nchini Tanzania na Pwani ya Msumbiji, ni ashirio kuwa ni suala la muda mfupi tu kabla ya teknolojia ya matumizi ya nishati hiyo kuenea katika eneo lote la Kusini mwa Jangwa la Sahara na kuchangia kuikomboa dunia kutoka utumwa wa kutegemea mafuta kutoka kwa 'Mashekh'."

"Mashekh," ikimaanishwa kuwa ni nchi za Uarabuni ambazo ni kitovu cha upatikanaji wa mafuta ya petroli duniani.

Katika medani za kimataifa, mpaka wakati huu nchi zinazotoa gesi kwa wingi duniani ni Urusi (asilimia 20 ya gesi yote duniani), Marekani asilimia 19, Canada (5), Qatar (4.5) na Iran ambayo huzalisha asilimia 4.

Uzalishaji wa gesi katika baadhi ya nchi nyingine chache zilizosalia upo chini ya asilimia 4.

Ingawa Urusi ndiyo mzalishaji namba moja wa gesi ya dunia, Marekani ndiyo inayoongoza kwa utumiaji bidhaa hiyo na ikifuatiwa na Urusi yenyewe.

Pia, lipo bomba kubwa kutoka Urusi kwenda Ujerumani, ambalo lilizinduliwa mwaka 2011 kwa ajili ya kusafirisha gesi ya kibiashara kwenda Ulaya Magharibi.

Vipimo vya bomba hilo ni kipenyo cha sentimeta 122 (inchi 48), urefu kilometa 1,222 na uwezo wa kusafirisha gesi yenye meta za ujazo bilioni 55 kwa mwaka.

Wakati huohuo Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA) linakadiria kuwa kuanzia mwaka huu 2013 China itashika nafasi ya tatu kwa matumizi ya gesi duniani, ambapo mpaka kufikia mwaka 2017 nchi hiyo itakuwa imevuka matumizi ya meta za ujazo bilioni 273.

Mwaka 2011 matumizi ya nishati ya gesi nchini China yalikuwa meta za ujazo bilioni 130, ambapo shirika la IEA linakadiria kuwa soko la gesi duniani litakua kwa asilimia 35, sawa na meta za ujazo bilioni 576.

Kiwango hicho kitaifanya dunia kuhitaji gesi ya meta za ujazo trilioni 4 katika kipindi cha miaka 5 ijayo kuanzia mwaka huu 2013, ambapo pia Marekani itaipita Urusi kwa uzalishaji wa nishati hiyo.

IEA inaeleza kuwa ifikapo mwaka 2035, matumizi ya gesi duniani yataongezeka na kuzidi yale ya makaa ya mawe ambayo kwa sasa yanashika namba mbili nyuma ya mafuta ya petroli.

Tanzania ikiwa mojawapo wa nchi zenye kuhodhi gesi nyingi, ni budi iwahi mapema kuweka mikakati ya uhakiaka (isiyo na mikataba mibovu) ili iweze kukamata sehemu ya juu katika soko la bidhaa hiyo duniani.

Takwimu hizo chache ambazo tumeweza kuzipata moja kwa moja kutoka makao makuu ya IEA mjini Paris, Ufaransa, zinaonesha jinsi gesi itakavyokua na soko pana duniani katika kipindi cha miaka michache ijayo.

Hivyo basi, pengine ni kutokana na ukubwa wa mradi huo ndio maana wananchi wa mkoa wa Mtwara waliandamana kutaka uwazi zaidi katika utekelezaji wake.

Inasikitisha kuwa Mkuu wa Mkoa huo wa Mtwara, Bw Joseph Simabakalia, anaripotiwa kuwa alikataa kwenda kuyapokea maandamano hayo ya amani na kuwasikiliza wananchi.

Waandamanaji wa Mtwara walitoa hoja 9 (wao waliziita ni maazimio) ambazo zilisomwa mbele ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vyama vya Siasa, Bw. Hussein Mussa Amir, wa chama cha TLP, ambaye aliyapoke maandamano hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Bw Joseph Simbakalia.

Waandamanaji walitaka kusikia kuwa kiasi fulani cha asilimia (hata kama ni kidogo) kutoka kwenye mauzo ya gesi kikatwa na kubakishwa kwenye Halmashauri za Wilaya za Mkoa huo ili kuendeleza sekta mbalimbali za umma, kama vile afya, elimu, miundombinu, na kadhalika.

Pia, waandamanaji walitaka kutekelezwa kwa vitendo ahadi ya Rais wao mpendwa, Jakaya Kikwete, aliyotoa mwaka 2009 wakati akiwa ziarani mkoani humo, ambapo, pamoja na mambo mengine, aliwataka watu wa mkoa huo kujiandaa kuwa Ukanda wa Viwanda.

Wananchi hao walitaka kusikia sababu zinazokwamisha utekelezwaji wa ahadi hiyo ya Rais wao, na ambaye (tunaamini) anayaelewa vyema matatizo ya kiuchumi ya mkoa huo, na hasa ikizingatiwa kuwa huu ni mwaka wa 4 tangu kutolewa ahadi hiyo.

Kadhalika, walitaka vijengwe vinu vikubwa vya kufua nishati ya gesi hapohapo Mtwara, badala ya kuisafirisha kwa njia ya bomba ikiwa katika hali ya umalighafi hadi Dar es Salaam.

Kwa upande mwingine, badala ya serikali kukwepa maandamano hayo ingejitokeza na kuuambia umma kwa ujumla jinsi ilivyo vigumu kujengwa kwa haraka vinu hivyo ambavyo ni budi kwanza kukamilika ndipo uvunaji wa gesi uanze.

Wanamtwara wangeambiwa kuwa kusimamisha uvunaji wa gesi kusubiri kukamilika ujenzi wa vinu hivyo kuna athari nyingi, ikiwemo nchi kuchelewa kuingiza "sokoni" bidhaa husika.

Umma wa Mtwara ungeambiwa kwamba ni vyema uvunaji wa gesi uanze kwanza wakati juhudi za kujenga vinu vikubwa zikiendelea.

Hiyo ni pamoja na kutafuta mtaji wa kujenga kinu kikubwa zaidi cha kuweza kutosheleza mahitaji yote ya ufuaji wa nishati hiyo kwa nchi zote za Kusini na Kati mwa Afrika.

Hoja hizo za waandamanaji zikiwa katika kurasa mbili zilisomwa na Katibu wa Umoja wa Vyama vya Siasa, Bw Seleman Litope, na ambaye aliitaka serikali ieleze athari za mazingira ambazo hutokana na uchimbwaji wa gesi.

Kadhalika, walitaka gharama za kuunganishiwa umeme wa TANESCO zipunguzwe mpaka kuwa sh. 50,000, ili kila mwananchi aweze kufaidika kutokana na uwepo wa gesi hiyo ambayo pia inahubiriwa kuwa itatumika kufua umeme na kuondoa uhaba wa nishati hiyo nchini.

Wananchi hao walitaka Serikali isitishe ujenzi wa njia ya bomba hilo kwenda Dar es Salaam mpaka madai yao yatakapopatiwa ufumbuzi.

Umma kwa ujumla ungefahamishwa kwamba nchi kusimamisha mradi mkubwa kama huo wa gesi, ambao tayari umeanza kutekelezwa, huitumbukiza katika hasara kubwa, hususan pale ambapo hulazimika kulipa fidia kwa makandarasi.

Kwa ufahamu wetu kuhusu sekta ya uvunaji wa mafuta ya petroli, gesi, maji, na nishati zinazotiririka, usafirishaji wa nishati kwa njia ya bomba ni husika kwa asilimia 100.

Kama kwamba hiyo haitoshi, gesi hainyonywi moja kwa moja kutoka kisimani na kusafirishwa. Ni budi kiwepo kiwanda ambacho kitatumika kuisindika ili kisafisha kabla ya kuisukuma kwa mitambo mikubwa ili isafiri kwenda sokoni.

Fedha ambazo zitapatikana zitaingizwa katika mfuko wa bajeti ya Serikali kwa matumizi ya Watanzania wote.

Mambo kama hayo ndiyo ya msingi na ambayo inatakiwa kufikishwa kwa umma waziwazi, kwani ni yenye maslahi kwao na taifa lao kwa ujumla.

Ni wajibu muhimu kwa viongozi wote katika kambi zote za vyama vyote vya siasa nchini, na wale wa Serikali, kuwaelimisha wananchi bila kuegemea kwenye uongo wa kisiasa. Uongo huo wa kisiasa hauna tija taifani.

No comments:

Post a Comment