21 January 2013

Waishitumu NASA kuficha sayari TishioNa Danny Matiko

MAKALA yaliyopita tuliwaletea habari za kukanusha madai ya kuwepo sayari tishio kwa dunia, hususan kufuatia uvumi uliosambaa duniani mwishoni mwa mwaka jana 2012, kwamba kulikuwa na sayari kubwa ikija kuigonga dunia na kuisambaratisha.


Katika Makala hayo ya utafiti kuhusiana na madai hayo, tuliweza kufuatilia kwa kina taarifa za taasisi maarufu za uchunguzi wa anga za juu ili kubaini kama kweli kulikuwa na tishio la aina hiyo, angalao kwa sasa.

Hata hivyo, katika utafiti huo ambao ulihusisha taarifa za Shirika la Safari za Anga za Juu la Marekani (NASA), Shirika la Utafiti wa Anga za Juu la Ulaya (ESA), la Urusi (ROSCOSMOS) na lile la China (CNSA), hatukubaini kuwepo sayari tishio kwa dunia.

Majibu kutoka mashirika hayo yalionesha kutokuwepo tishio la aina yoyote kutoka anga za juu, au zile za mbali, dhidi ya dunia.

Mantiki katika majibu hayo ni kwamba kama sayari hiyo tishio (kwa dunia) ingekuwa ipo katika uelekeo wa kutoka anga za mbali kuja duniani, ingeisha onekana iking'aa zaidi kuliko nyota zote.

Mashirika hayo yanaeleza kuwa umbali unaotenganisha sayari ni mkubwa, na, kwa maana hiyo, haiwezekani sayari tishio kuwa na mwendo kasi kuweza kufika duniani katika kipindi kisichozidi miaka takribani 10.

Katika hatua nyingine, hususan kufuatia kupoa kwa madai hayo ya kuwepo ujio wa sayari hatari kwa dunia, baadhi ya raia wa nchini Marekani wanalishutumu shirika la anga za juu la nchi hiyo, NASA, kwamba limekuwa likificha baadhi ya mambo ya anga ambayo umma una haki ya kuyafahamu.

Wanadai kuwa, kwa mfano, mwaka 1969 wakati wa safari za vyombo vya Apollo kwenda kutua mwezini, NASA ilificha baadhi ya mambo na pia kukanusha vikali baadhi ya madai yaliyotiliwa shaka, wakati yalikuwa ya kweli.

Mojawapo ni uvumi uliokanushwa na shirika hilo la kuchunguza anga ni madai kwamba mavazi waliyovaa wanaanga waliosafiri na vyombo hivyo yalikuwa yamewekewa mionzi hatari ya kinyuklia ili waitumie kujihami kwa kushambulia kitu cho chote ambacho kingewashukia ghafla, wakiwemo viumbe wa anga za juu kama wangekuwepo huko.

Baadhi ya wananchi hao wamekuwa wakidai kuwa mavazi hayo yalikuwa na mionzi, na kwamba vitufe vya kufyatulia mionzi hiyo huonekana dhahiri upande wa kifuani mwa kila mwanaanga hao.

NASA ilikanusha madai hayo na kueleza kuwa vitufe hivyo vilikuwa na kazi nyingi, ikiwemo kuwezesha mawasiliano na pia kuchukuwa vipimo vya kiafya kwa kila mwanaanga husika.

Wakati wa maadhimisho ya miaka 42 tangu binadamu wa kwanza alipotua mwezini Julai 20, 1969, Makala haya tulifuatilia madai hayo, ambapo licha ya kukanushwa na msemaji wa NASA kwa njia ya simu, pia tulifuatilia kwa njia ya mtandao ili kuona ulivyokuwa uundwaji mavazi hayo.

Tuliwaletea wasomaji wetu jinsi mavazi hayo yalivyotengezwa, ambapo pia tuliweza kufuatilia mpaka kwenye kiwanda kilichoyatengeneza na kuona fomyula iliyotumika kuyasuka.

Mavazi hayo ni kofia nene yenye miwani ambayo pia hufanyakazi kama kamera, simu na kinasa sauti, suruali iliyounganishwa na koti lake ambavyo kwa pamoja vimefungamanishwa na viatu mfano wa buti.

Mavazi hayo pia kwa ndani yaliwekewa sponji nene isiyopisha maji, joto, wala ubaridi visivyotakiwa. Pia upande wa mgongoni yaliunganishwa na mtungi wenye hewa ya oksijeni kwa ajili ya mwanaanga kupumulia.

Mavazi hayo rasmi sana kwa usalama wa wanaanga wa mwezini yalikuwa na uzito wa kilo 80 hapa duniani, lakini kule mwezini uzito huo ulipungua mpaka kuwa kilo 3.

Hivyo basi, tulifuatilia mpaka siku mavazi hayo yalipochukuliwa kiwandani na kupelekwa makao makuu ya NASA, ambapo jozi 3 za mavazi hazo zilikabidhiwa kwa mtuza stoo na kuhifadhiwa kwenye chumba maalumu.

Tulifuatilia mpaka siku mavazi hayo yalipoondolewa hapo stoo usiku wa kuamkia safari ya Apollo ya kwanza kwenda mwezini, ambapo yalipelekwa kwenye chumba cha kilichotumika kuwaaga wanaanga hao tayari kwa safari.

Kwa kuwa Apollo iliondoka saa 3:32 asubuhi, wanaanga walianza kujiandaa kuanzia saa 10 alfajiri, ambapo mojawapo ya majukumu ilikuwa ni pamoja na kuyavaa mavazi hayo kwa mara ya kwanza mbele ya kandamnasi ya viongozi wa NASA ili kuona kama wanaanga hao wangeweza kuyavaa wakiwa peke yao muda mfupi kabla ya chombo kuanza kutua mwezini.

Baada ya hapo wanaanga hao waliyavua mavazi hayo, ambapo yalibebwa na kuingizwa ndani ya Apollo ambayo ilikuwa tayari imeegeshwa mahali pa kuazia safari.

Katika hatua zote hizo za kushughulikia mavazi hayo, haikuoneshwa mahali popote kama yaliwekewa mionzi hatari ya nyuklia.

NASA walidai kuwa wachunguzi wao wa anga walikwishabaini kutokuwepo hatari yoyote huko mwezini, na hivyo hawakuwa na sababu ya kuwahami wanaanga hao kwa kutumia nyuklia.

Ilidaiwa kuwa tishio pekee la usalama wa Apollo hiyo ya kwanza ilikuwa ni kutoka kwa chombo cha anga kisichojulikana, maarufu kama UFO, ambacho kilijitokeza siku ya 3 Apollo ikiwa safarini huko anga za juu.

Mwanaanga Michael Collins ambaye alikuwa rubani wa Apollo anadai kwenye kitabu chake cha "Carrying the Fire" (kubeba moto) kwamba UFO ilijtokeza ghafla na kumudu kwenda nao sambamba kwa masafa marefu, licha ya Apollo kuwa katika mwendo kasi wa kilometa 40,000 kwa saa.

Anaeleza kuwa walipotoa taarifa duniani kwa makao makuu ya NASA kwamba kulikuwa na chombo kigeni kinawafuatilia, walijibiwa kuwa "hiyo ni UFO, achana nayo, zingatieni safari maana ndiyo muhimu kwenu." Baadaye UFO hiyo ilitoweka.

Kadhalika, shutuma nyingine dhidi ya NASA ni madai kwamba inaficha habari za UFO ambavyo ni vyombo ambavyo asili yake imebaki kuwa kama kitendawili. Rai wa Marekani hudai kuwa NASA wanafahamu ukweli kuhusiana na UFO hizo.

Katika shutuma za sasa dhidi ya NASA, baadhi ya raia wa Marekani wanadai kuwa kuna sayari ijulikanayo kwa jina la "Nibiru" ambayo wakuu wa shirika hilo wanaficha habari zake.

Raia hao wamekuwa wakidai kuwa sayari hiyo ni tishio kwa dunia, kwani hata zama za kale iliwahi kusababisha madhara makubwa kwa dunia.

"Nibiru" ambalo ni jina lenye asili ya nchini Irak ndilo huitambulisha sayari hiyo, ambapo maana yake kwa Kiswahili ni sayari "ipitayo" karibu na anga ya dunia.

Madai ya raia hao yanajengwa juu ya utafiti wa mwandishi wa habari, Zakaria Sitchin, raia wa Jamhuri ya Azerbaijan ambayo ni mojawapo ya Jamhuri za Taifa Kubwa la Urusi ya zamani (USSR) iliyosambaratika mwaka 1990.

Sitchin aliandika kitabu mwaka 1976 kiitwacho "The 12th Plnet" (sayari ya 12), ambapo alidai katika kitabu hicho kwamba kuna sayari kubwa huko anga za mbali ambayo hupita karibu na dunia kila baada ya miaka 3,600 na kusababisha kuchafuka kwa hali ya hewa duniani.

Katika machapisho yake yaliyofuatia madai hayo, mwandishi huyo alidai kuwa ugunduzi wake ulitokana na utafiti alioufanya nchini Irak ambayo ni eneo ulipoanzia ustaarabu wa dunia.

Alidai kuwa sayari ya Nibiru ilifahamika vyema kwa wenyeji walioishi ilipo nchi ya Irak ya sasa, ambapo pia hapo kale eneo hilo lilifahamika kama Mesopotamia, Babiloni na Tigris.

Kitabu hicho ambacho mwandishi huyu amekisoma chote kina maelezo ambayo ni vigumu 'serious thinker' yeyote (mwenye uwezo wa kutafakari usahihi wa mambo) hawezi kuyakanusha yote kwa mara moja.

Kuanzia Makala yajayo tutawaletea kwa kina habari za sayari hiyo, "Nibiru."
.

No comments:

Post a Comment