21 January 2013
Tuhoji polisi inapotumia mabomu kudhibiti sisimizi
Na Gladness Mboma
JUZI wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) wanaokaa katika makazi ya mtu binafsi Kigamboni waliandamana hadi Makao Makuu ya Polisi, ambako pia ni Makao Makuu ya Mambo ya Ndani kwa lengo la kutoa malalamiko yao juu ya vitendo vya kubakwa, kulawitiwa na kuibiwa mali zao na watu wanaodhaniwa majambazi mara kwa mara.
Kitendo cha wanafunzi hao kuandama ni kutokana na kudai kuwa walikwishatoa taarifa muda mrefu Kituo cha Polisi Kigamboni bila ya hatua zozote kuchukuliwa na kuhisi kuwa waalifu hao wanashirikiana na polisi.
Kuandamana kwa wanafunzi hao kulizua vurugu kubwa, ambapo baadhi ya wanafunzi wa kike na wakiume walidhalilishwa wakati walipokuwa wakienda kudai haki yao ya kimsingi.
Kitendo cha Polisi kuonekana hadharani wakiwapiga na hata kuwadhalilisha wanafunzi hawa hakipendezi, kwani hawakutakiwa kufanya hivyo hata kama walikuwa wanavurugu.
Hali kama hii inasababisha ukosefu wa amani nchini mwetu na hata kujikuta serikali ikichukiwa kwa jambo dogo ambalo limesababishwa na watumishi wake wenyewe.
Sasa imekuwa kama vile ni desturi kwa polisi wa Tanzania pale wanapotakiwa kutuliza fujo wao wanapiga sasa sielewi kwanini wafanye hivyo tena kwa wanafunzi ambao wanauwezo wa kuwadhibiti bila kutumia nguvu.
Ifike mahali sasa Polisi wetu mjifunze, kwani mmeshaleta madhara makubwa, lakini bado hamkumbuki, jirekebisheni Watanzania watawaogopa msitumie nguvu kubwa ambayo haitajiki.
Ninachotambua ni kwamba wajibu wenu ninyi polisi ni kulinda maisha ya raia na mali zao na siyo kuchukua sheria mkononi kama ambavyo sasa mmekwishazoea.
Sasa ninyi kama jeshi la polisi mkianza kuvunja amani ya nchi, nchi itatawalika kweli kama mmesahau taratibu zenu za kazi rudieni makabrasha yenu msome mjifunze tena mnachotakiwa kufanya ni nini na siyo kuchukua sheria mkononi.
Mmekuwa mkifanya vitendo vya uvunjifu wa sheria kila mara na jinsi Mungu alivyomkubwa picha zinaonyesha wazi wazi mapungufu yenu katika utendaji wa kazi zenu, hatuwezi kufika mbali kwa stahili hii, mtasababisha maafa kwa raia.
Narudia tena wanafunzi walikuwa na haki ya kuandamana kwa sababu walikuwa wanakwenda kudai haki yao ya msingi, hivyo hakupaswa kutumia mabavu katika kuwathibiti.
Wanafunzi hao ambao wanadai wameibiwa vifaa mbalimbali zikiwemo Kompyuta 300, simu za mkononi, kujeruhiwa pamoja na kubakwa na kulawitiwa waliwasilisha kwingine wanakoona kuwa watapatiwa ufumbuzi baada ya kuripoti kwa muda mrefu katika kituo husika bila ya kupatiwa ufumbuzi.
Mbali na hali hiyo hata mmiliki wa hosteli hiyo wakiwemo viongozi wa wanafunzi IFM walikwisharipoti matatizo hayo, lakini inaelekea Polisi wameamua kuwaacha wanafunzi hao kuishi maisha ya hofu na kuruhusu vibaka wafanye wanavyotaka.
Kuna jambo moja ninajiuliza ina maana watu wanapofanya maandano ni lazima polisi waibuke na silaha, maji ya kuwasha,mabomu na dhana zingine ina maana bila dhana hizo hawawezi kufanya kazi, tusifike huko hii ni nchi yenye amani na upendo tusianze vitisho hivyo kwa sasa bado sana nchi yetu bado ni changa.
Namshauri IGP Mwema kukaa pamoja na watumishi wake waelezwe kwamba wanachokifanya sicho, kwani wakiachiwa waendelee na mtindo wao wa kujeruhi, kudhalilisha watu itakuwa ni hatari.
Watanzania ni watu wapole na watulivu sana,kinachotakiwa kwa askari polisi wetu kuachana na ulinzi wa kutumia mabavu, ili kuepusha vurugu na matatizo mengine ambayo yanaweza kuvunjisha amani nchini.
Pili mkumbuke kwamba mnapokuwa mnawafanyia vitendo hivi wanafunzi wao wanachotambua ni kwamba mmetumwa na serikali, hali hii inasababisha kuongeza chuki dhidi ya wanafunzi na serikali yao.Ni vema tukaachana na nguvu za mabavu zenye kutaka kupitisha uvunjifu amani nchini.
Hivyo tunaomba msiwarudishe nyuma Watanzania wakaanza kufikiri matukio ya nyuma ya mauaji ya Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Channel Ten mkoani Iringa Bw. Daud Mwangosi ambacho kilisababishwa na kipigo kutoka kwa polisi.
Wakati naangalia juzi picha za wanafunzi wa IFM waliokuwa wakipigwa virungu na polisi bila huruma huku wengine wakiwa wanadhalilishwa nilianza kujiuliza hivi mna nini mbona Tanzania imegeuka mataifa ya nje yenye vurugu nilishindwa kupata jibu.
Msitufanye tuanze kuwaogopa,kwani ninyi mmewekwa kwa ajili ya kulinda raia na siyo kuwashushia vipigo kama ambavyo mnafanya sasa, ifike mahali mhachane na vitendo hivyo vya kidhalilishaji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment