14 January 2013

Katiba Mpya itoe adhabu kwa wanaokataa kuwatambua viongozi wanaochaguliwa


Na Suleiman Abeid

MFUMO wa uongozi nchini unaundwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 2005 ambapo viongozi wake hupatikana kwa njia ya kidemokrasia kwa kuchaguliwa na wananchi kupitia sanduku la kura.

Viongozi wanaochaguliwa katika nafasi mbalimbali kuanzia serikali za vitongoji, mitaa, vijiji, kata na majimbo ya uchaguzi akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wote hudumu katika nafasi hizo kwa kipindi cha miaka mitano ambapo uchaguzi mkuu hufanyika kila baada ya kipindi hicho.

Hata hivyo mgawanyo wa madaraka ya kiuongozi upo katika maeneo mawili makuu ambayo ni serikali za mitaa wanakochaguliwa wenyeviti wa serikali ngazi ya vitongoji, mitaa, vijiji na madiwani wa kata na sehemu ya pili ni ile ya Serikali Kuu ambako wabunge na Rais huchaguliwa.

Mgawanyo huo wa madaraka unatajwa rasmi na katiba ya sasa inayotumika nchini, sura ya nane ibara ya 145 (1) kuhusu Madaraka ya Umma inasema;

"Kutakuwa na vyombo vya serikali za mitaa katika kila mkoa, wilaya, mji na kijiji katika Jamhuri ya Muungano, ambavyo vitakuwa vya aina na majina yatakayowekwa na sheria iliyotungwa na Bunge au Baraza la Wawakilishi."

Katiba inatoa haki kwa kila raia anayetimiza sifa anaweza kuchaguliwa kuwa kiongozi katika nafasi yoyote ile na pale atakapokuwa ameshinda atatakiwa kula kiapo kabla ya kuanza rasmi kuwatumikia wananchi waliomchagua ambao ndiyo watakuwa waajiri wake kwa kipindi chote cha uongozi wake.

Ibara ya 21 ya Katiba (1) inafafanua haki hiyo, nanukuu: "Bila ya kuathiri masharti ya ibara ya 39 ya 47 na ya 67 ya katiba hii na ya sheria za nchi kuhusiana na masharti ya kuchagua na kuchaguliwa, au kuteua na kuteuliwa kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi,"

"Kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa hiari yao, kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria,"mwisho wa kunukuu.

Hata hivyo pamoja na katiba hiyo (ambayo kwa sasa huenda ikaandikwa mpya) kutoa haki hiyo kwa kila raia, bado kuna watu au makundi ya watu kwa misingi ya kisiasa hukataa kuwatambua viongozi wanaochaguliwa kihalali kwa matakwa yao ya kisiasa.

Hali hii imechangia kwa kiasi kikubwa wananchi katika baadhi ya maeneo mengi nchini kukosa maendeleo waliyoahidiwa kutokana na malumbano ya kisiasa ambayo kiundani mara zote huwa hayana maslahi yoyote kwa wapiga kura wa eneo husika.

Kwa kawaida madiwani na wabunge wanaochaguliwa kwa mujibu wa katiba na kanuni za uchaguzi kabla ya kuanza kuwatumikia rasmi wananchi waliomchagua wanapaswa kula kiapo cha utii na baada ya kiapo hicho hutambulika rasmi kama viongozi halali hivyo mtu anapokataa kuwatambua anakuwa amevunja katiba.

Katiba yetu nchini inaelekeza wenyeviti wa vitongoji, mitaa, serikali za vijiji, madiwani na wabunge akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano, atokane na vyama vya siasa lakini baada ya kuchaguliwa kuapishwa rasmi lazima wawatumikie wananchi wote bila ya kujali itikadi ya vyama vyao.

Hali hiyo ndiyo imewasukuma wakazi wa miji ya Mwandoya na Mwanhuzi wilayani Meatu mkoani Simiyu kupendekeza katiba ijayo iweke kipengele kitakachotoa adhabu kali kwa watu wote wanaogoma kuwatambua viongozi wanaochaguliwa kihalali na wananchi kupitia sanduku la kura.

Wanasema tabia ya baadhi ya watu kugoma kuwatambua viongozi wanaochaguliwa kisheria hasa upande wa madiwani na wabunge imechangia kwa kiasi kikubwa kuchelewesha maendeleo ya wananchi kutokana na mivutano inayochangiwa na masuala ya kisiasa.

Alex Emmanuel mkazi wa Mwanhuzi mjini anasema ili kuondoa malumbano yasiyo na maana kila baada ya kumalizika kwa chaguzi za madiwani na wabunge ni muhimu sasa katiba ijayo iweke kipengele cha sheria kitakachowezesha kushtakiwa kwa watu wote wanaokataa kuwatambua viongozi waliochaguliwa kisheria.

"Mimi nashauri ili kuondoa malumbano ya wanasiasa katiba ijayo iweke ibara itakayoruhusu watu wote wanaokataa kuwatambua madiwani na wabunge ambao wamechaguliwa kihalali, wakatangazwa na wakala viapo vya kuwatumikia wananchi, basi washtakiwe na wafungwe gerezani,"

"Baadhi ya kata na majimbo ambayo madiwani wake na wabunge wanatokana na vyama vya upinzani hivi sasa kumekuwepo na matatizo makubwa sana, wanasiasa ambao wagombea wao walishindwa katika uchaguzi wa mwaka 2010 wamegoma kabisa kuwatambua watu walioshinda, sasa hii kimaendeleo inakuwa tatizo."

Wanasema iwapo patakuwepo na sheria hiyo, ni wazi hapatakuwepo na vikwazo vya maendeleo katika kata na majimbo ambayo madiwani na wabunge wake hawatokani na vyama vya siasa vilivyopo madarakani.

Kwa upande wake Joshua Kalando anapendekeza katiba ijayo ifafanue wazi muda wa Rais aliyeko madarakani uwe unakoma sambamba na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linapovunjwa rasmi baada ya kukamilika kwa kipindi chake cha miaka mitano.

Anasema, utaratibu wa hivi sasa wa Rais kuendelea na wadhifa wake hata baada ya bunge kuvunjwa umechangia kwa kiasi kikubwa Rais anayemaliza muda wake kuvunja katiba Ibara ya 38 kifungu kidogo cha (2) (a) ambacho kinaeleza kwamba, nanukuu;

"(2) Bila ya kuathiri masharti  mengineyo ya katiba hii, kiti cha rais kitakuwa wazi na uchaguzi wa rais utafanyika au nafasi hiyo itajazwa vinginevyo kwa mujibu wa katiba hii, kadri itakavyokuwa kila mara litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo: (a) baada ya bunge kuvunjwa," mwisho wa kunukuu.

Anasema uzoefu unaonesha kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano amekuwa akiendelea kuhesabika kama rais wa nchi hata baada ya kuvunjwa kwa bunge la Jamhuri ya Muungano hali ambayo ni kuvunja katiba ambapo hudiriki hata kuteua watendaji wa serikali akiwa katika kipindi cha kampeni.

"Kwa kweli Rais kuendelea na madaraka yake hata kipindi cha kampeni anakuwa anavunja katiba ya nchi, ni vyema katiba mpya iweke mkazo kwamba baada ya kuvunjwa kwa bunge na madaraka ya rais aliyeko yakome papo hapo, anapoendelea kuhesabika kama rais, katika kipindi cha kampeni hupata upendeleo na ulinzi mkubwa kama rais wa nchi," anasema Kalando.

Anasema ni muhimu Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini ikalifanyia kazi suala hili kwa kuangalia kwamba baada ya bunge kuvunjwa na kukoma kwa madaraka ya rais aliyeko madarakani, ni mtu au chombo gani kikabidhiwe jukumu la kusimamia nchi mpaka pale rais mwingine atakapochaguliwa na kuapishwa rasmi.

"Kwa hili lazima katiba mpya iliwekee mkazo, linaminya demokrasia ya kweli nchini, maana kwa mujibu wa ibara ya 41 (1) ya katiba ya sasa iliyopo, baada ya bunge kuvunjwa vyama vyote vya siasa vinakuwa na haki sawa ya kusimamisha wagombea wao katika kuwania nafasi hiyo."

Kwa upande wao wakazi wa mji mdogo wa Mwandoya wanasema katiba ijayo iwazuie watendaji wa serikali wakati wa kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu au uchaguzi mdogo wasishiriki katika kampeni hizo kama inavyofanyika hivi sasa.

Wanasema ushiriki wa watendaji wa serikali hasa wale wenye nyadhifa za kisiasa mfano wa mawaziri mara nyingi hutumia nyadhifa zao kuwatisha wananchi kwa kudai wasipomchagua mgombea wa chama kilichoko madarakani hawatapata maendeleo.

Mwakilishi kutoka Jukwaa la Katiba nchini, Obeid Mkina aliyekuwa mwezeshaji katika midahalo iliyoandaliwa na Azaki ya MENGONET wilayani Meatu, amewataka wakazi wa wilaya hiyo kuthamini kura zao wanazopiga kuchagua viongozi katika chaguzi mbalimbali.

"Lakini pia mbali ya kuthamini kura hizo, ni vizuri wananchi mkajiepusha na tabia iliyozoeleka miongoni mwenu ya kuombaomba fedha kutoka kwa wagombea, fedha hizo mnazopewa zina athari kubwa katika suala zima la maendeleo,"

"Tabia hii husababisha diwani au mbunge kutotimiza wajibu wake kikamilifu akiamini kikifika kipindi cha uchaguzi  atatumia tena utaratibu ule ule wa kugawa fedha ili achaguliwe kwa mara nyingine na hivyo kutoona umuhimu wa kuwatumikia kikamilifu wapiga kura wake," anasema Mkina.

Mwenyekiti wa MENGONET wilayani Meatu, Esther Joseph anasema Azaki yake inaendesha midahalo hiyo kwa ufadhili wa Shirika la The Foundation For Civil Society kwa lengo la kujenga mahusiano kati ya wananchi, madiwani na wabunge, anasema midahalo hiyo pia imetoa fursa kwa wakazi wa wilaya hiyo kutoa maoni yao juu ya katiba mpya inayotarajiwa nchini.

No comments:

Post a Comment