21 January 2013

Marufuku mifuko ya jamii kujenga bila mikataba-POAC



Anneth Kagenda na
Rachel Balama

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC),imeipiga marufuku Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii kujenga miradi yoyote bila kuwa na mikataba kwani kufanya hivyo kunaweza kuleta madhara siku za usoni.


Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa kamati hiyo Bw.Zitto Kabwe wakati ikipitia ripoti ya Mfuko wa Pensheni wa (LAPF), ambapo alisema kuwa katika majibu ya Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo Eliud Sanga, alisema kwa kawaida huwa wanajenga miradi na baadaye inafuata mikataba.

"Kauli hii ya mazoea ya kujenga miradi alafu badaye mnaandika mikataba na kupeleka hazina ili iwalipe kamati haitakubaliana nayo, unasema serikali inafanya vizuri kwenye malipo au huwa mnajenga kwa kawaida yenu je siku serikali ikibadilika nani atakulipa,"

"Lakini pia katika kupitia ripoti zenu kwa haraka inaonesha mifuko hii mnataka kugeuza fedha za wananchi kuwa ka-TRA kadogo kwani hatuwaelewi mtu unaanzaje kujenga na baadaye unaenda kudai kwanini usiingie makubaliano kwanza," alihoji Zitto.

Alisema, kuwa tatizo lingine linaloweza kujitokeza ni kwamba wakati mifuko hiyo ikiendelea kudai mabilioni yake inaweza kuingia serikali nyingine kwenye madaraka jambo linaloweza kuwa na utata zaidi huku akihoji kuwa ikiwa hivyo wataenda kumdai nani au kushtakiwa mahakama gani.

Hata hivyo walikemea suala la kuonekana fedha hewa kama lilivyojitokeza ambapo sh. milioni 43 zilionekana zimeandikwa lakini haijulikani zimefanya nini.

Naye Mjumbe wa Kamati hiyo Kangi Lugola, alisema kuwa katika suala la kuandikwa fedha na zisionekane ni kuiongopea kamati.

"Kitendo cha kutwambia fedha hii haijulikani ilipo eti kwa sababu mlikuwa mnatoka kwenye mfumo mmoja kwenda kwa mwingine ni kuiongopea kamati vitendo hivi hatutakubaliana navyo," alisema.

Katika hoja mbalimbali zilizotolewa ndani ya kamati hiyo Mkurugenzi Sanga, alisema pamoja na kuwapo madeni mbalimbali lakini hivi saa Chuo cha Serikali za Mitaa cha Hombolo Mkoani Dodomo kimekamilika hivyo Serikali inadaiwa sh. bilioni 34.

  

No comments:

Post a Comment