04 January 2013

TCDD: Deni la taifa limefikia sh. trilioni 22


Na Goodluck Hongo

MTANDAO wa Madeni na Maendeleo nchini (TCDD), umesema deni la Taifa limefikia sh. trilioni 22 wakati deni la nje sh. trilioni 15.9 hadi kufikia Oktoba 2012, ambapo deni hilo ni sawa na bajeti ya Serikali kwa mwaka mmoja na nusu.

Mkurugenzi Mtendaji wa TCDD, Bw. Hebron Mwakagenda, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema deni hilo limeongezeka kwa dola za Marekani milioni 456.1 sawa na asilimia 4.5, katika kipindi cha mwaka mmoja tangu Oktoba 2011 na kuvuka viwango vya kimataifa.

“Ni vyema suala la ukopaji likawekwa katika Katiba Mpya, takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zinaonesha deni la ndani limefikia sh. trilioni 5.1 au dola za Marekani bilioni 3.2 hadi kufikia Oktoba 2012, sawa na ongezeko la sh. bilioni 513 sawa na asilimia 10 tangu Oktoba 2011,” alisema Bw. Mwakagenda.

Alisema deni la ndani linakuwa kwa kasi kutokana na Serikali kuanza kukopa kwenye benki za biashara ambazo zinatoza riba kubwa ambapo hali hiyo imewafanya wachumi kuonesha wasiwasi wao juu ya mwendendo wa nchi inavyoendelea kukopa.

Aliongeza kuwa, hofu ya wachumi ni juu ya Serikali kutumia fedha nyingi bila kupata ruhusa au kibali cha Bunge, nidhamu ya kukopa na matumizi ya fedha hizo pamoja na hali ya deni kuvuka kiwango cha kimataifa.

Bw. Mwakagenda alisema, athari za kuendelea kukua kwa deni
la Taifa ni nyingi ambazo ni pamoja na uwezekano wa nchi kutoaminika kukopesheka kama kutakuwa na uhitaji wa lazima.

Athari nyingine ni uwezekano wa nchi kushindwa kulipa madeni kwa wakati na kutoaminika tena machoni mwa wakopaji, kuvuruga uimara wa shilingi, kuzidisha mfumuko wa bei.

Alizitaja athari nyingine ni uwezekano wa kutumika kwa mwanya wa kukopa ili baadhi ya maofisa na watendaji serikalini ambao si waaminifu kujilimbikizia mali kwa kuzingatia mikataba mingi
haina udhibiti wa kibali cha Bunge. 

“Awali kila kiongozi alikuwa na uwezo wa kukopa kisheria lakini hivi sasa anayetakiwa kukopa ni Waziri wa Fedha akiwa na kamati yake lakini deni limefikia kiasi hiki.

“Waziri wa Fedha Dkt.William Mgimwa aache siasa katika suala hili bali anapaswa kutueleza kwanini deni hili ni endelevu kwani nchi haiwezi kukopesheka kama deni litakuwa kubwa.

“Sisi tunatumia viwango vya kimataifa kama GDP kujua ukubwa
wa deni tulilonalo kama Taifa, deni la Tanzania lilipanda kutoka dola za Marekani bilioni 1.83 mwaka 2010 hadi dola za Marekani bilioni 2.3 mwaka 2011,” alisema Bw. Mwakagenda.

Aliongeza kuwa, Tanzania lazima ijifunze kutoka nchi za Ulaya kama Ugiriki, Ugiriki, Hispania na Ireland ambao madeni yao si endelevu tena na wako katika matatizo makubwa kiuchumi kutokana na madeni makubwa waliyokopa.

“Kam deni limerejea katika kiwango cha kuzidi kile tulichokuwa tunadaiwa kabla ya msamaha ni fedheha na aibu kwa Taifa hivyo
ni wazi kuwa tumeanza mwaka 2013 na deni kubwa,” alisema.

Alisema fedha zinazokopwa na Serikali zinakwenda katika ujenzi wa madaraja, barabara, kulipa mishahara ya wafanyakazi na mbaya zaidi zinakopwa kwenye benki za biashara na Mashirika ya Hifadhi za Jamii kama NSSF.

No comments:

Post a Comment