04 January 2013

Morani 'wajifua' kupambana na askari



Na Lilian Justice, Kilosa

VIJANA wa Kimasai (morani), waliopo katika Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro, wameanza mazoezi ya kupambana na askari watakaoendesha operesheni ya kuwaondoa wafugaji ambao wanadaiwa kuvamia maeneo wilayani humo.

Kutokana na hali hiyo, viongozi wa jamii ya wafugaji wapo katika wakati mgumu wa kuwatuliza vijana hao ili kuepusha machafuko yanayoweza kutokea wakati operesheni hiyo itakapoanza kutekelezwa.

Wakizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika mkutano wa wafugaji kwenye Kijiji cha Mbwande, wilayani humo, mmoja wa viongozi hao ambaye ni Katibu wa Chama cha Ushirika kijijini hapo, Bw. Paul Sauyaki, alisema operesheni hiyo imelenga kuwaondoa wafugaji waliopo katika Bonde la Kilombero.

“Kazi kubwa inayofanywa na viongozi wa kimila katika jamii ya Kimasai ni kutuliza hasira za Morani ambao wanadaiwa kutaka kupambana na watendaji watakaofanya operesheni ya kuwaondoa wafugaji waliovamia katika Wilaya hii.

“Operesheni hii imepangwa kuanza hivi karibuni na imelenga kuwasaka na kuwaondoa wafugaji wanaodaiwa kuvamizi sehemu mbalimbali za vijiji vya Wilaya ya Kilosa wanaotokea Kilombero na Ulanga ambapo kuna operesheni ya kuwaondoa wafugaji,” alisema.

Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa la Calvary, Israel Kilwaha alisema migogoro mingi inayoibuka wilayani humo kwa kuhusisha wafugaji na wakulima, inasababishwa na Serikali.

Alisema hali hiyo inatokana na wafugaji kukosa maeneo ya kulishia mifugo yao na kama Serikali ya Wilaya ya Kilosa isingetoa ranchi kwa wawekeza wa nje, ingepunguza migogoro hiyo kwa kutoa maeneo ya ranchi hizo kwa wafugaji ambao ni wenyeji.

“Ukiangali kwa umakini utaona Serikali imekuwa ikifanya mambo mengi bila kushirikisha wahusika katika mambo mbalimbali lakini kwa upande wa wafugaji, hizi ranchi zilizotelekezwa na Shirika la Taifa la Chakula na Kilimo (NAFCO), wangepewa wafugaji wenyeji.

“Badala yake Serikali ambayo ndio inayopaswa kutatua mgogoro huu imezitoa ranchi hizi kwa wawekezaji wageni hivyo ni vigumu migogoro hii kupatiwa ufumbuzi,” alisema Mchungaji Kilwaha.

Aliongeza kuwa, kitendo hicho kinachangia iliyopo ambapo wafugaji ambao ni wenyeji wana uwezo wa kuzinunua kwani wawekezaji hao hawaziendelezi.

Alisema hasira za Morani zinatokana na kukumbuka upotevu wa mifugo yao katika operesheni iliyofanyika mwaka 2009 ambayo iliwakumba wafugaji wenyeji na wavamizi.

Akizungumzia malalamiko hayo, Mwenyekiti wa Halmashauri  ya Wilaya ya Kilosa, Amer Mbaraka, alisema operation hiyo imelenga kuwaondoa wafugaji wavamizi waliotoka wilayani za Kilombero na Ulanga ambao wanadaiwa kuingia katika wilaya hiyo na haiwezi kuwaathiri wafugaji wenyeji kama inavyodhaniwa.

Wilaya ya Kilosa imetoa notisi ya siku 10 kuanzia Desemba 2012 ambapo operesheni hiyo ilitarajiwa kuanza jana.

No comments:

Post a Comment